Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amehimiza Asasi za kiraia ziwe mstari wa mbele kwa kushirikiana na Serikali kuelimisha umma kuhusu kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia ili jamii iishi kwa upendo na kujenga Uchumi wa nchi.
Akizungumza Wilayani Kwimba katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalikofanyika ki mkoa Wilayani humo,Mhe.Malima amesema bado kunahitajika jitihada za kutosha za kuelimisha umma hasa kutokana na matendo ya ukatili kwa Wanawake kuzidi kushamiri hali inayotishia kuja na kizazi kijacho kisicho staarabika.
"Wanawake ni nguzo imara sana katika kuchangia Uchumi wa nchi,na wamekuwa mfano mzuri wa kurejesha mikopo wanayopata kwenye Halmashauri,unapo mtenga mwanamke kiuchumi,kisiasa au shughuli yoyote ya kijamii hatari yake ni kubwa,"amesema Mhe.Malima.
Aidha, Mhe.Malima amewataka wazazi kujenga utamaduni wa kuwa karibu na watoto wao na kuzungumza nao mara kwa mara hali ambayo itawasaidia kujua mapema mienendo michafu inayowakabili.
"Watoto wengi wamekuwa mbali na wazazi wao kwa kuwaogopa, huku wakikabiliwa na vitendo vichafu hii siyo sawa tubadilike, amesisitiza Mhe. Malima.
"Rais wetu Mhe.Dkt. Samia ameonesha mfano wa mwanamke shupavu wa kupigania maendeleo ya Taifa letu, amewapa na anaendelea kutoa nafasi mbalimbali za uongozi kwa Wanawake,wajibu wenu msimuangushe na badala yake mchape kazi kwa bidii kwa kuiga mfano wake," ameongeza Mhe.Ng'wilabuzu Ludigija Mkuu wa Wilaya ya Kwimba.
"Tusisahau kuwekeza kwenye familia zetu, Serikali ya awamu ya Sita imepania kumuinua mtoto wa kike katika mabadiliko ya teknolojia, zitajengwa Shule maalum za kuwapa kipaumbele wanafunzi wa kike ili wasiwe nyuma katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia, kwa hiyo tusijisahau kuziunga mkono juhudi hizi," amesema Mhe.Anjelina Mabula Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
"Kila ifikapo Maadhimisho haya tuyatumie kujipima harakati zetu mbalimbali kwa lengo la kusonga mbele katika nyanja mbalimbali ili tufike katika malengo letu tuliyonuia," amesema Mhe.Merry Masanja Naibu Waziri Mali Asili na Utalii.
Katika Maadhimisho hayo wakina mama wajawazito kutoka kata 30 za Wilaya ya Kwimba wamekabidhiwa majiko ya Gesi kwa lengo la kumuondolea mwanamke adha ya kutumia muda mrefu kusaka kuni.
Kila ifikapo Macho 8 Dunia huadhimisha siku ya Wanawake huku chimbuko lake likiwa ni kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji dhidi yao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.