Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka viongozi wa vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCCOS) kuimarisha ushirika na kudhibiti dalili zote za ufisadi.
Mhe.Mongella ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mauzo ya trekta kutoka Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) mkoani hapa.
"Jambo la msingi ni kuziba mianya yote na kutorejea nyuma kwa kuwa kilichomaliza ushirika huko nyuma ni ufisadi,"alisema Mongella.
Aidha alisiaitiza kuwa ili kukuza uchumi wa wanachama na kubadilisha maisha ya wananchi ni vyema wakishirikiana kwenda kwenye kilimo cha biashara chenye tija na kuondokana na kilimo cha jembe la mkono kwani asilimia 80 ya wakazi wa Mwanza wanajihusisha na kilimo.
"Hii kazi ya kuuza matrekta tutaifanya Lakini maofisa wenu na wa benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania wachangamke kufikia September 1 mwaka huu lazima hizi trekta 27 zilizopo ziwe zimeondoka," alisema Mongella.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la taifa la maendeleo Dkt. Samuel Nyantahe alisema mradi huo wa kiwanda cha kuunganisha matrekta unatokana na ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamuhuri ya Poland mkataba huo ulisaniwa septemba 28 mwaka 2015.
"Serikali ya Poland ilitoa mkopo nafuu wa dola za marekani milioni 110 kwa riba ya asilimia 0.3 kwa mwaka ambapo mkopo huo utatumika kwa asilimia 100 kugharamia ununuzi wa vifaa na huduma kutoka Poland kuja Tanzania, " alisema Dkt.Nyantahe.
Aidha Dkt.Nyantahe amesisitiza kuwa lengo la mkopo huo ni kuboresha kilimo nchini kinachoendana na uchumi wa viwanda, hadi sasa matrekta 779, kati ya 2,400 yameshaingizwa kutoka Poland ambapo matrekta 432 yameshaunganishwa.
Naye Ofisa mwandamizi msimamizi wa mradi na Tathimini kanda ya ziwa Stephen Kang'ombe alisema lengo lao ni kuwatoa wananchi katika kilimo cha kujikimu hadi kibiashara na kutoka kwenye matumizi ya jembe la mikono hadi kilimo cha kisasa kwa kutoa mikopo iliyo na riba nafuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Emmanuel Kipole alisema wao wamejipanga kuchukua matrekta mengi ili kuboresha kilimo, uzalishaji wa mazao hasa ya pamba kwa kiasi kikubwa.
" Mwaka hadi mwaka tumekuwa tukiongoza kwa uzalishaji lakini kwa kutumia dhana hizohizo duni sasa tutatumia dhana hizi za kisasa ili kuboresha kilimo kutokana na mahitaji yetu kuwa makubwa, " alisema Kipole.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.