RC MTANDA AAGIZA KUONGEZWA KWA VIFAA NA NGUVUKAZI KUKAMILISHA UJENZI KITUO CHA MICHEZO MALYA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka kampuni ya CRJE (East Africa) Limited inayojenga mradi wa kituo cha michezo cha umahiri Malya Wilayani Kwimba kuongeza nguvukazi na vifaa ili kuharakisha ujenzi huo.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo Januari 13, 2025 wakati alipofanya ziara chuoni hapo na kusema Mkandarasi alipaswa kukamilisha mradi huo tarehe 16 mwezi huu kwa mujibu wa mkataba lakini ameshafanya kazi kwa asilimia 14.7 tu na kumpa onyo kwamba Serikali haitomvumilia endapo atachelewesha mradi huo.
Ameongeza kuwa, Serikali imetenga fedha zaidi ya Tshs. Bilioni 31 ili kuimarisha sekta hiyo nchini kwa kupata vifaa na miundombinu ya kisasa hivyo mkandarasi hatovumiliwa atapoonekana na lengo la kukwamisha juhudi hizo.
" Mkandarasi au mtu yeyote aliye hapa anaweza kujionea kwa macho ya kawaida tu kwamba vifaa na nguvukazi zilizopo hapa havioneshi dhamira ya kutaka kukamilisha mradi huu kwa haraka, sasa naagiza muongeze kabla sijawachukulia hatua."
Katika kufuatilia hilo kwa karibu, Mhe. Mtanda amemtaka mkandarasi kuketi pamoja na mshauri, uongozi wa Wilaya na chuo na kuwekeana ratiba ya kazi ambayo itafuatwa kila wakati na kuhakikisha wanaifuata na kuitekeleza.
Awali, msimamizi wa mradi huo mhandisi Feisal Msingwa alibainisha kuwa mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali Tshs. Bilioni 3.1 na muda wa utekelezaji wa mradi huo ni mwaka mmoja (Miezi 12) kutoka Januari 2024 hadi Januari 2025 lakini alisimama kazi kwa muda wa miezi minne kutokana na ucheleweshaji wa malipo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.