RC MTANDA AAHIDI KUWA MLEZI BORA KWA MAAFISA USAFIRISHAJI WA SERIKALI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amefungua kongamano la Maafisa usafirishaji wa Serikali mkoani humo na kuwaahidi kuwa mlezi bora wa chama chao ili kiweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Akizungumza nao leo Machi 2, 2025 kwenye ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa Mtanda ambaye ni mlezi wa chama hicho amewakumbusha maafisa hao wa usafirishaji kuendelea na kutimiza wajibu wao wa kulinda usalama barabarani.
"Afisa usafirishaji tambua wewe ni mtu muhimu, tanguliza nidhamu kwa mkuu wako wa kazi, tunza siri na siku zote hakikisha chombo chako ni salama kabla ya kuanza kukitumia", Mkuu wa mkoa.
Vilevile, mlezi huyo amewataka baadhi ya viongozi wenye tabia ya kuwanyanyasa madereva kama vile kuwatumia muda mwingi pasipo sababu, kuingilia posho za mafuta waache tabia hiyo kwani haina tija zaidi ya kujenga chuki.
Aidha, katika mkutano huo Mkuu huyo wa Mkoa amekipongeza chama hicho kwa kuzidi kujiimarisha kwa kuwa na wanachama wengi kutoka idadi ya 80 hadi 183 na kawataka wale ambao bado hawajajiunga kutoka Ofisini kwake wafanye hivyo haraka.
"Nimesikia katika risala yenu baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa Ofisi na kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi yenu,natoa maelekezo kwa Katibu Tawala kukaa na uongozi wenu ili kupatikane ufumbuzi na kikao kijacho nipate mrejesho",Mtanda.
Awali katika taarifa yake fupi kwa mgeni rasmi,Katibu wa chama hicho Mkoa,Juma Mago amebainisha bado wanachangamoto kwa baadhi ya waajiri kuwa wagumu kutoa ruhusa kuhudhuria mikutano yao pia amempongeza mlezi wao kwa kuwajali kwa vitendo hali iliyowafanya kuhudhuria kwa wingi katika mkutano wao wa Taifa uliofanyika mwaka jana Jijini Arusha.
Katika kongamano hilo RC Mtanda amekabidhiwa tuzo kutokana na mchango wake bora kwa maafisa usafirishaji wa Serikali mkoani Mwanza,na pia baadhi ya Taasisi za Serikali zimekabidhiwa vyeti kutokana na ushirikiano mzuri wanaotoa kwa chama hicho na wanachama wake
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.