RC MTANDA ACHANGIA MIL.5 MATIBABU YA WATOTO WENYE SARATANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo septemba 17, 2024 amechangia kiasi cha shilingi milioni tano katika kampeni ya kuwachangia watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya saratani (Bugando Health Marathon 2024).
Sambamba na mchango huo, Mhe. Mtanda pia ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani humo kuungana na Hospitali ya Kanda ya Bugando katika kampeni ya kuwachangia watoto hao ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa fedha za matibabu.
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa mchango na rai hio alipokutana na Wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mwanza watakaoshiriki Bugando Health Marathon 2024 itakayofanyika tarehe 20 Oktoba, 2024 iliyolenga kuchangia fedha za matibabu kwa watoto wanaokabiliwa na maradhi ya saratani.
Aidha RC Mtanda amesema Hospitali ya Bugando wao wameamua kuisaidia Serikali kwa kuwa serikali haiwezi kufanya kila kitu hivyo ushiriki wa kampeni hiyo itasaidia kupunguza mzigo kwa serikali.
"Utafiti unaonesha kwamba Mkoa wa Mwanza umekuwa na changamoto ya Watoto wengi wanaokabiliwa na maradhi ya saratani na saratani hizi zikitibiwa mapema basi inaweza kutibika lakini matibabu yake ni gharama sana hivyo ndio maana nimewaiteni ili mtusaidie kutuunga mkono tuweze kuwasaidia watoto wetu". Amesema RC Mtanda.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kanda Bugando Dkt. Fabian Massaga amesema wamedhamiria kukusanya takribani kiasi cha Shilingi Bilioni moja ambapo inakadiriwa kusaidia watoto takribani mia tano wanaokabiliwa na maradhi hayo.
Kadhalika Dkt. Massaga amewaomba wadau hao kujitoa kwa kuwaunga mkono na kubainisha kuwa sadaka watakayoitoa ni thawabu kwao na kwa hao watoto ambao nai wana ndoto za kuishi na kuwataka pia kushiriki katika mbio hizo zinazotarajiwa kuongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.