RC MTANDA AFAFANUA UKWELI WA KILICHOTOKEA SIKU YA MAZOEZI YA SIMBA-CCM KIRUMBA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda amekanusha taarifa ya uongo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayotolewa na msemaji wa klabu ya Simba,Ahmed Ally kuwa ameingilia mazoezi ya Simba akiwa pamoja na askari wenye silaha na kuwataka wananchi na mashabiki kuipuuzia taarifa hiyo yenye nia ya kumchafua na kumvunjia heshima.
Mkuu huyo wa Mkoa amelazimika kuzungumza na vyombo vya habari mapema leo asubuhi Novemba 22,2024 Ofisini kwake baada ya kupokea ujumbe mwingi wa kuulizwa kuhusiana na uzushi huo,na kubainisha alichofanya yeye kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa ni kwenda uwanjani baada ya kupokea taarifa ya kutaka kupigwa na makomandoo wa Simba na kujifungia vyumbani wasimamizi wa Pamba Jiji kwenye uwanja huo ili wasiumizwe na kuanza kuvunja vioo vya madirisha.
Mtanda amesema anatambua kanuni za soka na asingeweza kuingia uwanjani wakati ilikuwa ni siku ya mazoezi ya Simba na badala yake alikuwa nje ya uwanja akifanya mawasiliano na baadhi ya viongozi wa Simba ili wazungumze kuachiwa wasimamizi wa Pamba Jiji waliokimbilia vyumbani kuhofia kupigwa na makomandoo wa Simba.
"Jitihada zangu za kuzungumza na viongozi wa Simba ziligonga mwamba nikiwa nje ya uwanja hadi walipomaliza mazoezi yao na mlango kufunguliwa na askari kuingia na kuwafikisha kituo cha polisi aliyevunja vioo vya madirisha na wasimamizi wa Pamba Jiji kwa maelezo zaidi",amefafanua Mkuu wa Mkoa.
Ameongeza kuwa kutokana na sakata hilo Mwenyekiti wa klabu ya Simba Murtaza Mangungu baadaye alimpigia simu na kumuomba radhi kwa yote yaliyotokea na kuahidi kugharamia hasara iliyotokea ya uharibifu uwanjani hapo.
Mtanda amewaondoa hofu mashabiki wote na kuwataka kuendeleza mshikamano wa amani na kufurahia burudani ya kuzishuhudia timu kubwa za Simba na Yanga na kupuuzia uzushi huo ulioenezwa na msemaji wa klabu ya Simba Ahmed Ally ambao una nia ya kuwapa taharuki mashabiki kuelekea mchezo huo utakayopigwa leo Novemba 22,2024 kwenue uwanja wa CCM Kirumba.
Aidha Mtanda amebainisha yeye ataendelea kuwa mlezi na kushirikiana na timu mbalimbali licha ya mahaba yake ya kuipenda Yanga kwani hivi karibuni aliwachangia fedha tawi la Simba walipokuwa wanajiandaa na tamasha la Simba Day na amekuwa mlezi wa matawi yao sehemu mbalimbali alizofanya kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.