RC MTANDA AFANYA MAZUNGUMZO NA GAVANA WA JIMBO LA JIANGSU-CHINA, AKARIBISHA UWEKEZAJI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amekutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa Jimbo la Jiangsu kutoka China Mhe. Xu Kunlin na kumfahamisha fursa mbalimbali za uwekezaji ukiwemo ufugaji wa kisasa wa samaki, viwanda na Utalii.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Novemba 20, 2024 kwenye ukumbi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa, Mtanda amebainisha fursa nyingine zilizopo Mwanza ni madini na maeneo ya kufungua vyuo kwa ajili ya ufundishaji wa lugha ya kichina itakayosaidia wageni wa kitalii kutoka nchini humo.
"Hapa Mwanza tayari kuna mwekezaji kutoka China anayefuga samaki kwa njia ya vizimba na kutengeneza fedha nyingi,hivyo nawakaribisha mfike kwa wingi kuwekeza,"amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wakati akizungumza na ujumbe ulioongozana na Gavana huyo.
Mtanda amesema uhusiano kati ya Tanzania na China ulioasisiwa tangu mwaka 1961 na Hayati Julius Nyerere na Mao Tsetung umezidi kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Gavana Mhe.Kunlin ameonesha kufurahishwa na taarifa za Mkoa wa Mwanza ambao amesema jina la Rock City umefanana na la Jimbo lake linalojulikana kama Stone Town,na kuongeza kuwa amevutiwa na uwekezaji wa ufugaji samaki,kiwanda cha chakula cha samaki na utalii
"Nitakaa na uongozi wa ngu kwa ajili ya kufanya utafiti mzuri wapi eneo mwafaka kwa ajili ya kuja kuwekeza na kuzidi kuimarisha uhusiano wa majiji ya Mwanza na Jiangsu,"Mhe.Kunlin.
Gavana huyo na ujumbe wake wakiwa nchini kabla ya kuja Mwanza wamefanya pia ziara kisiwani Zanzibar lengo likiwa kuimarisha uhusiano na kuona fursa za uwekezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.