RC MTANDA AFANYA ZIARA STENDI YA MABASI NYEGEZI, ATOA MAAGIZO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda leo Aprili 9, 2025 amefanya ziara fupi kwenye stendi ya mabasi Nyegezi na kutoa maagizo kadhaa yakiwemo mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya stendi hiyo.
Akizungumza na Maafisa usafirishaji na watoa huduma mbalimbali ndani ya stendi hiyo iliyopo wilayani Nyamagana, Mkuu huyo wa mkoa amesema hakuna sababu ya wadau hao wa usafirishaji kufungua stendi zisizo rasmi wakati tayari Serikali imejenga miundombinu ya kisasa.
"Serikali imetumia zaidi ya Tshs bilioni 18 kwa ajili ya kujenga stendi hii ya kisasa ili wananchi wapate huduma bora, sasa kuwepo na stendi zisizo rasmi huko pembezoni kunaszbabisha Serikali kukosa mapato", Mhe. Mtanda.
Amebainisha Ofisi yake ipo mbioni kukutana na wadau hao wa usafirishaji sm pamoja na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ili kuweka mkakati imara ya uboreshaji wa huduma ndani ya stendi hiyo.
Aidha Mhe.Mtanda ametoa maagizo kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambao ni wamiliki wa kitega uchumi hicho kurekebisha kasoro zote ambazo ni kero kwa watoa huduma ndani ya stendi hiyo ukiwemo ushuru wa holela,ubovu wa barabara za kuingia stendi na ukosefu wa maji ya uhakika.
"Nimesikia malalamiko kutoka kwa maafisa usafirishaji,wananchi na watoa huduma,nakuagiza meneja wa stendi hii rekebisha kasoro hizo haraka iwezekanavyo tofauti na hapo nikirejea tena hapa na kusikia malalamiko yaliyojirudia nitakuwajibisha",amesisitiza mkuu huyo wa Mkoa.
Kuhusu ujenzi wa kituo cha Polisi ambacho kimeishia hatua ya boma,Mtanda ameutaka uongozi wa Jiji kukutana na wadau ili kukusanya nguvu ya pamoja kwa lengo la kukikamilsha na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.