RC MTANDA AHIMIZA KULIOMBEA TAIFA, KUTENDA MEMA NA KUWAKUMBUKA WASIO NA UWEZO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Aprili 10, 2024 ameungana na waumini wa dini ya kiislamu katika swala ya Eid iliyofanyika kwenye uwanja wa Nyamagana na kuwakumbusha kuendelea kuliombea Taifa kujenga mshikamano, kutenda matendo mema na kuwakumbuka wale wasio na uwezo na hatimaye kupata thawabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Taifa la Tanzania limeendelea kuwa na amani kutokana na busara na hekima za viongozi wetu wa juu hivyo hakuna budi kuwaombea ili Mwenyezi Mungu awazidishie ari ya kuwatumikia vizuri Watanzania.
"Wapo baadhi ya watu wanapokuwa kwenye nafasi huzitumia vibaya iwe kwa dhuluma au uonevu wa aina yoyote mambo ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu aliyetuleta Duniani ili tumtumikie vyema na kurejea kwake tukiwa wasafi wa roho," Mkuu wa mkoa.
Mara baada ya kushiriki swala ya Eid Mhe. Mtanda akiongozana na Shekhe Mkuu wa mkoa wa Mwanza Hassan Kabeke pamoja na wadau benki ya NMB wakiwa kwenye Ofisi za Bakwata mkoa, wametoa zawadi ya sikukuu kwa vituo 11 vya watoto wanaoishi katika mazingira magumu kutoka wilaya Nyamagana na Ilemela zenye thamani ya shs milioni 2.6
"Mhe.mkuu wa mkoa tunakushukuru sana kwa tendo hili,hizi fedha ulizogharamia pengine ungeamua kula vizuri na familia yako,lakini ukaamua kuzitoa kwa ajili ya wengine,Mwenyezi Mungu azidi kukupa rehema zake," Shehe Kabeke.
Akimshukuru mkuu wa mkoa kwa zawadi hizo, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi amesema watoto hao wanaendelea kujiona ni wa famllia moja kutokana na Jamii kuwa nayo karibu kwa kuwapa misaada mbalimbali.
Akiwa katika Iftar iliyoandaliwa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe.Hassan Masala Jumanne hii jioni kwenye Hotel ya City Link,mkuu huyo wa mkoa amesema Ofisi yake ipo wazi wakati wote kuwasikiliza wale wenye kero mbalimbali.
"Mimi siyo mkaaji wa ofisini bali nitawafuata huko mlipo wananchi na wale mtakaofika ofisini kwangu mjisikie huru kuniona lakini sitaki kuletewa taarifa chonganishi," amesisitiza Mhe.Mtanda wakati akitoa hotuba fupi mara baada ya Iftar.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.