RC MTANDA AHIMIZA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA MAPATO YA NDANI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Halmashauri ya Jiji la Mwanza kutumia fedha za mapato ya ndani kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuhakikisha zinapelekwa kwenye miradi ya maendeleo ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 15 Julai, 2024 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza wakati akizungumza na Viongozi wa Serikali, watumishi na wadau wa maendeleo wilayani Nyamagana.
Mtanda amesema, kwa mujibu wa makusanyo ya fedha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024 halmashauri hiyo inapaswa kupeleka shilingi Bilioni 10 kwenye miradi ya maendeleo lakini wamepeleka Bilioni 8 hivyo ameagiza kupelekwa kwa bilioni 2 zilizobaki.
"Ukitaka kujua mimi ni nani, chezea fedha za miradi, yaani mradi usipokamilika wakati fedha zipo ni lazima nikupeleke TAKUKURU, sitakuacha maana hauwatakii mema wananchi ambao wanasubiri huduma kutoka kwenye miradi inayotekelezwa." Amesisitiza Mhe. Mtanda.
Vilevile, amewapongeza Halmashauri hiyo kwa kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kila mwaka huku akitolea mfano ongezeko la kutoka shilingi Bilioni 17 (2022/23) hadi Bilioni 24 (2023/24) ambayo ni asilimia 88 ya malengo pamoja na uhodari wa kujibu hoja za mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali.
Naye Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Amina Makilagi pamoja na mambo mengine amebainisha changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi kama uhaba wa maji hususani kwa maeneo ya Buhongwa, Lwanhima, Igoma na Butimba na akamuomba kiongozi huyo wa mkoa kushughulikia.
Upungufu wa vyumba vya madarasa 1632, matundu ya vyoo 3807 na madawati 17771 kwa elimu ya awali na msingi ni miongoni mwa changamoto alizozitaja na akabainisha mikakati mbalimbali ya kukabiliana nazo ambazo wanaendelea kushughulikia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.