RC MTANDA AHIMIZA UKAMILISHWAJI KWA WAKATI MIRADI YA KIMKAKATI, AAHIDI USHIRIKIANO NA WAWEKEZAJI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Mei 16, 2024 amefanya ziara kukagua miradi ya kimkakati iliyopo wilayani Ilemela na kuhimiza ikamilike kwa wakati na kuahidi ushirikiano na mazingira mazuri kwa Wawekezaji.
Akianzia ziara hiyo kwenye ujenzi wa Kituo cha Kikanda cha kuratibu, utafutaji na uokoaji majini kinachomilikiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichogharimu Bilioni 59, Mtanda amemtaka mkandarasi CK Associates Co. Ltd kukamilisha ndani ya muda waliokubaliana kwenye mkataba ambao ni hadi mwezi wa 11 mwaka huu.
"Ofisi yangu ina wajibu wa kufuatilia na kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati na yenye ubora ili iwe na tija kwa wananchi na eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki", Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Mtanda baada ya kutoa maagizo hayo alisogea uwanja wa ndege na kukagua jengo la abiria, mizigo na sehemu ya kuongozea ndege na kushauri fedha za mradi huo shs bilioni 28 ziletwe Ofisi za TAA Mwanza ili kuwe na huduma za haraka kila zitakapo hitajika na mkandarasi badala ya kuwepo makao makuu ya Mamlaka ya viwanja vya ndege.
"Tayari mashirika sita ya ndege za kimataifa yamewasilisha maombi ya kuja kutoa huduma hapa, tunahitaji uwanja wa ndege wa Kimataifa hakuna sababu ya kufumbia macho aina yoyote ya ucheleweshwaji wa mradi huu, fedha za kazi za awali shs bilioni 12 tayari zipo kwa utekelezaji, mkandarasi amesema anaanza kazi Jumatatu na iwe hivyo," RC Mtanda.
Meneja wa uwanja wa ndege Mussa Mchola amesema tayari Mkandarasi Taifa Construction yupo Site na anafanya matayarisho na muda wake wa ujenzi kwa mujibu wa mkataba ni miezi 11.
Mkuu huyo wa Mkoa akiwa ameambatana na uongozi wa Halmashauri ya Ilemela wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,Mhe.Hassan Masalla amefika kwenye Karakana ya Songoro Marine inayojenga vivuko 5 vya Serikali vyenye gharama ya shs bilioni 28 vitakavyotoa huduma Ukerewe na Misungwi.
Mara baada ya kupatiwa taarifa fupi na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Meja Songoro iliyo muomba Mkuu huyo wa Mkoa kusaidia uharaka wa malipo,Mtanda ameahidi kuzungumza na Waziri wa Fedha na wa Uchukuzi ili fedha ziletwe kwa wakati shs bilioni 8 hadi 10 ili zikamilishe miradi hiyo na wananchi wapate huduma bora na salama ya usafiri wa majini.
"Jana nimeshuhudia mwenyewe wakazi wa Ukerewe na Kisorya wanavyo taabika na shida ya usafiri kutokana na Kivuko cha Mv Ujenzi kuwa na hitilafu ya injini na kuagiza Kivuko kutoka Sengerema kwenda kusaidia wananchi usafiri,"
Aidha ameipongeza Kampuni ya Songoro ambayo ni ya kitanzania kwa kufanya kazi kizalendo licha ya changamoto ya uchelewashaji wa malipo lakini karibu kazi zote zipo hatua ya mwisho.
Mkuu wa Mkoa Mhe.Mtanda amehitimisha ziara hiyo siku ya leo kwa kutembelea Kampuni ya Uchenjuwaji wa Madini yenye hisa kwa Serikali 25% na Muwekezaji kutoka Dubai 75% yenye gharama ya shs bilioni 16.
Mtanda amesema Serikali imeweka mazingira mazuri kwa Wawekezaji na bado Mwanza fursa za uwekezaji zipo nyingi Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wakati wote.
"Hongereni Shirika la Madini STAMIKO hii ni hatua nzuri na inaleta heshima kwa Taifa letu ya dhahabu za viwango zinazotoka hapa,"amesema Mhe.Mtanda.
Mkurugenzi wa Utawala kutoka STAMIKO,Deusdedit Magalla amebainisha kutokana na uwekezaji wa mitambo ya kisasa kwenye Kampuni hiyo wamekuwa wakitoa dhahabu ya kiwango cha Kimataifa na kukubaliwa na nchi yoyote Duniani kutokana kwenda na thamani ya fedha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.