Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kusimamia ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ili iweze kutoa huduma zilizokusudiwa kwa wananchi.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo Julai 28, 2025 wilayani humo wakati akikagua miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ambapo imegharimu fedha mbalimbali kutoka Serikali kuu, mapato ya ndani pamoja na nguvu za wananchi.
Akikagua mradi wa kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Maligisu amewaagiza RUWASA kuzitendea haki milioni 530 zilizotolewa na serikali kuu kwa kuhakikisha wanakamilisha mradi huo mara moja ili uhudumie wakazi zaidi ya 8000 wanausubiria.
Aidha, amewaagiza watendaji wa vijiji kupanga bei na wananchi ili kuwa na umiliki na ushirikishwaji wa pamoja jambo litalosaidia kuutunza mradi huo ipasavyo pamoja na kuingiza maji kwenye nyumba zao na kulipia ankara za maji.
Akikagua ujenzi wa Bweni la wanafunzi lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika shule ya sekondari Ngudu linalogharimu Milioni 160 Mkuu wa Mkoa ameagiza urekebishaji wa kasoro ndogondogo na ukamilishaji wa haraka wa bweni hilo.
Vilevile, amemuagiza Afisa Elimu wa Mkoa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupitia kwa kutumia gesi ya asili na mbadala inayopatikana kwenye mazingira ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuepusha uchafuzi wa mazingira kama walivyofanya kwenye shule ya Ngudu.
Kabla ya kukagua mradi wa Daraja la Sasi linalojengwa kwa Tshs. Bilioni 5.5 Mkuu wa Mkoa ameagiza mkandarasi anayejenga nyumba 1 ya mtumishi (Wakuu wa Idara) kati ya mbili zinazojengwa kwa Tshs. Milioni 160 kila moja kuhakikisha anarekebisha kasoro kwenye njia ya kuingilia walemavu na nyufa kwenye kuta.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.