RC MTANDA AKAGUA UWANJA CCM KIRUMBA, AMPA SIKU 7 MENEJA KUREKEBISHA KASORO ZILIZO JITOKEZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 11 Machi, 2025 amekagua miundombinu ya uwanja wa CCM Kirumba na akamtaka Meneja wa uwanja huo kurekebisha kasoro zilizojitokeza
Akiongea baada ya ukaguzi huo, Mhe. Mtanda amesema amejiridhisha na hali ya miundombinu kwenye maeneo yote ya eneo la kuchezea, vyoo, eneo la watu mashuhuri pamoja na vyumba vya kupumzika wachezaji na kwamba hali ni nzuri.
Aidha, amesema amebaini upungufu wa mabenchi kwenye maeneo ya wachezaji kubadilisha nguo na kupumzika na eneo la kuchezea mpira kwenye maeneo ya magoli zilizopungua nyasi na akaagiza ndani ya siku saba warekebishe kasoro hizo.
"Msimamizi wa Uwanja huu tambua kuwa huu uwekezaji na kwenye biashara yoyote lazima uzingatie ubora wa huduma, sasa nakuagiza tumia vema wakati huu ligi imesimama kuboresha uwanja kwa kuondosha kasoro ndogondogo kama kurejesha mabenchi." Mhe. Mtanda.
Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa ameishukuru Bodi ya Ligi nchini kwa usimamizi mzuri wa michezo na ameahidi Serikali kuendelea kushirikiana na mamlaka husika nchini katika kuendeleza mchezo wa soka.
Awali, Mratibu Mkuu wa michezo ya ligi Mkoa Bwana Goodluck Nyawandi alibainisha kasoro nne za maji kuingia kwenye eneo la kupumzikia wachezaji, upungufu wa viti vya kudumu kwenye maeneo ya kupumzikia wachezaji na la watu mashuhuri na uwepo wa maji ya kudumu kwa matumizi ya kawaida.
Naye, Meneja wa Uwanja ndugu Hassan Ally amebainisha kuwa uongozi unaendelea kuboresha miundombinu hiyo na kwamba ndani ya juma moja watakamilisha ikiwemo uwekaji wa nyasi kwenye maeneo ya magoli ambazo zitawasili ndani ya siku 2 kutoka Arusha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.