RC MTANDA AKUTANA NA KUZUNGUMZA NA WAFANYABIASHARA MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Juni 26, 2024 amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Wafanyabiashara wa Mkoani humo lengo likiwa ni kuwasikiliza michango na maoni yao juu ya mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea Jijini humo
Katika mazungumzo yake Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wafanyabiashara wote waliofunga maduka yao kuhakikisha wanayafungua kwa hiari yao wenyewe kwani Serikali ya Mkoa wa Mwanza ipo tayari kuwasikiliza kama wana hoja za msingi.
"Kama wafanyabiashara mna hoja za msingi njooni tuwasikilize nimekwisha fungua milango kwa makundi yote njooni ofisini mtushauri na mlete hoja zenu na sisi tutaangalia namna sahihi ya kuwasaidia".
"Na kama mkileta hoja zenu zikawa zipo nje ya uwezo wetu sisi tutazipeleka kwa wakubwa wetu huko juu na wao watatupa maelekezo au wao watayatolea maelekezo wao wenyewe," Ameongeza RC Mtanda.
Akizungumza mara baada ya kuwasikiliza Wafanyabiashara hao wanaolalamikia utitiri wa kodi kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhe. Mtanda amesema hakuna Taifa linaloweza kujiendesha bila kodi, Serikali inakuwa na uwezo wa kuwahudumia na kupeleka miradi kwa wanachi kutokana na michango inayotolewa na wananchi wenyewe ikiwemo ulipaji kodi.
"Leo hii Serikali ya Rais samia inafanya miradi mikubwa hapa nchini, je angewezaje kutekeleza hayo kama sio kupitia makusanyo ya kodi kutoka kwa wananchi wake, maendeleo mengi yamefanyika hapa nchini kutokana na ya makusanyo ya kodi," Amesema RC Mtanda.
Mhe. Mtanda pia amesisitiza kuwa endapo wafanyabiashara hao wanataka sheria za kodi zibadilishwe basi hawana budi kuleta maoni yao ili wabunge wayachukue na wakayafanyie kazi bungeni maana chombo pekee kinachoweza kuunda na kuvunja sheria ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.