RC MTANDA AMEWATAKA WANANCHI KUDUMISHA AMANI NA KUFANYA KAZI KUJITAFUTIA MAENDELEO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi kuimarisha amani na kufanya kazi kwa bidii ili kujitafutia kipato na kuweza kuinua kipato na uchumi wao.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo jioni Juni 07, 2024 kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Misasi katika kata ya Misasi wilayani Misungwi ambapo alibaini uwepo wa vijana wavivu wasioshiriki kazi za kuleta maendeleo na badala yake wanajihusisha na uhalifu.
"Nataka kuona hatua kali zikichukuliwa dhidi ya wananchi wahuni wanaoharibu amani ya watu wengine kwa kujihusisha na wizi, kucheza Pool Table, ujambazi na uvutaji wa bangi na kila aina ya uhalifu" Mtanda.
Akisisitiza kuhusu umuhimu wa kulinda amani, Mhe. Mtanda ametumia wasaa huo kuwaonya Sungusungu ambao hutumika kama askari wa jadi wanaozuia uhalifu kuacha tabia ya kuwakamata na kuwapiga wahalifu badala yake wawafikishe kwenye vyombo ya sheria.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuacha kuingiza mifugo kwenye shamba la Serikali la mifugo la Mabuki kwani kufanya hivyo kunaharibu juhudi za Serikali za kuinua sekta ya mifugo kwa kuwaletea shamba darasa na ameagiza kutungwa kwa sheria ndogo kali kwa ajili ya kuwaadhibu wanaolisha mazao.
Mwalimu Diana Kuboja, Afisa Elimu wa Sekondari amewapongeza wananchi wa Mwasagera kwa kujenga shule ya sekondari kwa nguvu zao kwa asilimia 100 na imesajiliwa na kwamba ifikapo Julai 01, 2024 watoto wataanza kusoma kwani itafunguliwa.
Dkt. Clement Morabu, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa kutokana na uchakavu wa kituo cha Afya wamepeleka ombi maalum la kufanyiwa ukarabati na upanuzi wa kituo hicho na kwamba kwa sasa wamejengewa Jengo la Mionzi kutokana na fedha kiasi walizozipata.
Awali, Diwani wa Kata ya Misasi Mhe. Daniel Busalo amenainisha kuwa ndani ya kata hiyo wameshapokea fedha zaidi ya Bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na zaidi ya milioni 194 kutokana na fedha za ushuru yaani mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Awali, Bi. Veronica Heneriko mkazi wa kijiji cha Misasi ameelezea kero ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana ambapo amebainisha kuwa wanatumia dawa za kulevya hususani bangi na kwamba wanateseka na adha ya maji na kwamba ni kijiji cha Manawa pekee ndio wanaopata maji.
Martine Mashamba kutoka kijiji cha Mwasagera ameelezea changamoto ya watoto kufuata elimu ya Sekondari kwa umbali mrefu kutokana na kijiji hicho kukosa Shule ya Sekondari na kulazimika watoto kutembea hadi kijiji jirani na kusababisha utoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.