RC MTANDA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA MRADI WA UJENZI WA KAMPASI YA TAASISI YA UHASIBU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameridhishwa na ubora, kiwango na kasi ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Kampasi ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kanda ya Ziwa, unaotekelezwa katika Kata ya Nyangomango Wilayani Misungwi.
Akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo leo Julai 10, 2024, Mhe. Mtanda amesema mradi huo umemvutia sana na unapendeza hata kwa macho ambapo pia amesema uwepo wa Taasisi hiyo kumechagiza kuzaliwa kwa ajira mbalimbali kwa wakazi wa Nyangomango, Misungwi na Mwanza kiujumla.
"Mradi ni mzuri sana lakini lazima tuwe na mikakati ya kuboresha huduma za miundombinu, tunataka kuwepo na kituo hapa cha kusimama na kupakia abiria ili hata hawa bodaboda, bajaji na usafiri mwingine waweze kupata ajira".Mtanda
Sisi tunahitaji kuona kituo kimekamilika kabla ya wanafunzi hawajafika hapa, hatuhitaji maneno maneno, tunahitaji utekelezaji wa maelekezo, kwa hiyo hilo ninaamini mtalitekeleza kama mlivyosema mtaanza na kituo cha muda. Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha Mhe.Mtanda ametoa maagizo kwa Mamlaka ya udhibiti wa usafiri wa ardhi (LATRA) na wakala wa barabara za Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanatenga bajeti ya utengenezaji wa miundombinu ya kudumu ya barabara za kuingia na kutoka chuoni hapo ili mwakani barabara hizo zianze kutengenezwa.
Kadhalika Mkuu wa Mkoa amemuhakikishia Mkuu wa Chuo na wananchi wa Usagara na Misungwi kuwa Serikali ya Rais Samia imejipanga kwenye sekta ya maji kwa kuamua kuwekeza fedha zaidi ya Tshs. Bilioni 70 ambapo tayari chanzo cha maji kimeshajengwa na baada ya hapo kitakachofuata ni kusambaza huduma ya maji kwa wananchi.
"Sasa hivi tumepata bilioni 49, mkandarasi anarudi kazini kwa ajili ya kupanua miundombinu ya usambazaji maji na wananchi wa usagara wote watapata maji na hiki chuo pia kitapata maji",amesisitiza mkuu huyo wa mkoa
Akitoa Taarifa ya ujenzi wa kampasi hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza Dkt. Honest Kimario, amesema ilianzishwa mwaka 2021 katika Kataya Nyakato Wilayani Ilemela lengo ikiwa ni kusogeza huduma kwa wakazi wa kanda ya ziwa.
Lakini kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa huduma za Taasisi kwa wananchi ambapo hapo awali walikua wamepanga wameamua kunununua kiwanja hicho ndani ya Wilaya ya Misungwi chenye ukubwa wa mita za mraba 148,000 sawa na hekari 61 kwa ajili ha ujenzi wa miundombinu ya kudumu.
"Mwaka 2022 Taasisi ilipata fedha kiasi cha Tsh. Bilioni 7.8 kutoka Wizara ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kudumu na taasisi ilianza mradi 22.01.2022 na mradi unatarajiwa kukamilika 21.07.2024." Amesema Dkt. Kimario.
Mradi huo umeshakamilika kwa 98.5, aidha unajumlisha madarasa yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1100 kwa wakati mmoja ndani yake kutakua na maabara na maktaba ya kisasa ambapo jumla kuu ya wanafunzi wanaoweza kuhudumiwa kwa wakati mmoja ni 4650 kwa siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.