Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameshuhudia tukio la ushushaji kwenye maji Kivuko cha MV Bukondo kilichogharimu Bilioni 4.7 katika karakana ya Songoro Marine wilayani Ilemela ambayo inatarajiwa kwenda kusafirisha wananchi na mizigo kati ya Kisiwa cha Bukondo na Bwiro wilayani Ukerewe.
Akizungumza baada ya kushuhudia ushushaji huo leo tarehe 16 Septemba, 2025 ambao ni sehemu ya kazi itakayofanyikwa kwa vivuko vinne (4) Mkuu wa Mkoa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo kujenga vivuko vitakavyosaidia usafiri na usafirishaji.
Amesema, Mwanza yenye eneo la maji kwa asilimia 53 inategemea sana usafiri wa majini hususani kwa wananchi wa visiwani hivyo serikali kuwajengea vivuko vya kisasa itasaidia kuwaondolea adha ya usafiri na hatari ya ajari za majini walizokua wakizipata kutokana na kutumia mitumbwi.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kuvipokea na kuvitunza na kwa wataalamau watakaoviendesha amewataka kwenda kufanya kazi kizalendo ili kulinda fedha nyingi ambazo serikali imewekeza kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.
Mkurugenzi wa vivuko TEMESA Makao Makuu Mhandisi Lukombe Kingāombe amesema Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba tani 100, abiria 200 na magari madogo 10 na kwamba ujenzi umefikia asilimia 98 na mkandarasi amelipwa asilimia 80 ya mradi ambayo ni zaidi ya Bilioni 4.
Ushushaji wa kivuko hicho leo tarehe 16 Septemba, 2025 ni sehemu ya Vivuko 4 kikiwemo cha MV Ukerewe kitakachofanya kazi kati ya Kisiwa cha Rugezi na Kisorya wilayani Ukerewe ambacho kitashusha kesho Septemba 17, 2025 (Zaidi ya Bilioni 6) na vingine vitafuatia na hadi mwezi Novemba vitaanza kutoa huduma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.