RC MTANDA ASISITIZA UIMARISHWAJI WA UMOJA NA MSHIKAMANO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa rai kwa jamii kuendeleza umoja na mshikamano kwa kuwa Taifa la Tanzania limejengwa kwa misingi ya umoja bila ya kutanguliza tofauti zilizopo miongoni mwa jamii zetu.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo jioni ya leo Mei 12, 2025 alipokuwa akitoa salamu za Mkoa katika Ibada maalum ya kuliweka Wakfu jengo jipya la Kanisa la Waadventista Wasabato la Kirumba lililopo Wilaya ya Ilemela na kusema kuwa katika Tanzania hakuna dini, kabila au wananchi ambao ni bora kuliko wengine.
“Leo sote ni mashahidi shughuli hii ni ya Waadventista lakini pia masheikh na kofia zao wapo hapa, kwa nini? kwa sababu wao hawaoni kwamba ni bora kuliko nyie, hii ndio maana halisi ya mshikamano”.
Aidha Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Viongozi wa Dini kwa nafasi kubwa waliyonayo katika kukuza amani na utulivu amewawasihi kuendelea kuisaidia Serikali katika kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kulindwa hapa nchini.
Pia Mkuu wa Mkoa amewaomba Viongozi wa Dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhimiza jamii kuzingatia kuwa na mienendo inayoendana na Utamaduni, mila na desturi za Kitanzania ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Mbali na hayo, Mhe. Mtanda ametoa pongezi kwa Kanisa hilo licha ya kuendelea kuwajenga na kuwasaidia Watanzania kiroho, wamekuwa pia wakiwasaidia kimwili kwa kuwawezesha kupata maji safi na salama, elimu na huduma za afya na kuwaomba pia kuisaidia Serikali katika kuboresha hali za kiuchumi za Waumini wao na Watanzania kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.