RC MTANDA ATAKA GHARAMA ZA MAJI KUWA RAFIKI KWA WANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewaagiza Wakala wa Maji vijijini (RUWASA) Mkoani humo kushirikisha wananchi kupitia vikao kupata bei za Maji zilizo rafiki kwa hali zote ili lengo la miradi hiyo kusaidia jamii litimie.
Ametoa kauli hiyo leo jumatano tarehe 18 septemba, 2024 akiwa kwenye Kijiji cha Kahangara Wilayani Magu wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ukarabati maji uliotekelezwa na serikali kupitia Mradi wa Uviko 19 kwa zaidi ya Tshs. Milioni 508.
Mhe. Mtanda amewataka RUWASA kupitia wasimamizi wa jumuiya za watumia maji kutokupandisha bei za maji kiholela kwani kwa kufanya hivyo ni kwagombanisha wananchi na Serikali yao na kuwataka kuendelea kutoza bei ambazo ziliamuliwa na mikutano ya kijiji tu na si vinginevyo.
Mhe. Mtanda amesema serikali ya awamu ya sita inatekeleza miradi ya huduma za jamii hususani Maji kama unavyotarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 34 hadi 90 hivyo watendaji ni lazima wasimamie ukamilifu wa hilo.
Aidha, amewataka RUWASA kuhakikisha kuwa kupitia mradi huo wanafikisha huduma za maji kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijapata maji safi na salama ndani ya kata hiyo na kusimamia miundombinu hiyo ili maji yaendelee kutoka kila siku.
Meneja RUWASA Wilaya ya Magu Mhandisi Daud Amlima amebainisha kuwa mradi huo umeshakamilisha vituo 34 vya kuchotea maji ambayo vinatoa maji na kwamba unasimamiwa na wananchi wenyewe kupitia jumuia zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.