RC MTANDA AUTAKA UONGOZI WA ATCL KULETA NDEGE ZAIDI MWANZA KUBORESHA USAFIRI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda ameutaka uongozi wa Shirika la ndege nchini ATCL kuongeza idadi ya ndege mkoani humo kutokana na idadi ya abiria kuzidi kuongezeka hali inayosababisha kuwepo na ugumu wa kupata usafiri huo kirahisi.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa rai hiyo leo Julai 03, 2024 wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa chumba maalum cha abiria wa daraja la juu la biashara iliyofanyika eneo la uwanja wa ndege, Mtanda amebainisha kutokana na Jiji la Mwanza kuwa eneo la kimkakati ongezeko la usafiri wa anga limezidi kuongezeka.
"Mkurugenzi Mhandisi Matindi nalisema hili mbele yako, sasa hivi ukitaka kuondoka leo hii kutoka Mwanza kwenda Dar siyo rahisi kupata usafiri ni lazima ufanye utaratibu siku mbili kabla, sasa hii katika soko la ushindani itawaletea shida," amesema Mtanda.
Mkuu huyo wa Mkoa amezitaka Shirika hilo kuzidi kujiimarisha na kuepuka usitishaji wa safari kiholela ili kuzidi kujiaminisha kwa huduma bora kwa wateja wake, kwani mashirika makubwa ya kimataifa ndege yatakapoanza safari zake kuanzia uwanjani hapo waweze kuumudu ushindani.
"Nampongeza Rais Samia kwa kuendeleza mazuri kwenye Shirika hilo yaliyofanywa na watangulizi wake, ametoa shs bilioni 13 kujenga jengo la kisasa la abiria, hivi sasa mkandarasi Taifa yupo eneo la ujenzi kulikamilisha jengo hilo litakalo chukua abiria wa kigeni 600 kwa mkupuo na wazawa 800," Mhe. Mtanda.
Aidha Mtanda amelishauri ATCL kuona umuhimu wa kuweka safari ya moja kwa moja kutoka Mwanza hadi Makao makuu ya nchi Dodoma, kuliko ilivyo sasa abiria kulazimika kushukia Dar na kwenda Dodoma.
"Haiwezekani kushindwa kuwepo na muunganiko wa safari ya moja kwa moja kwenda makao makuu ya nchi ni lazima muone hadhi ya Dodoma na wapo abiria wengi wanaohitaji usafiri huo," amehimiza Mtanda wakati wa hafla hiyo fupi.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema wanatambua mchango mkubwa wa kibiashara wa Mkoa wa Mwanza na wapo katika mkakati wa kuboresha usafiri kutokea mkoani humo
"Hivi sasa tuna ndege 14 na tupo mbioni kupata ndege nyingine moja, tuna imani changamoto zilizopo zitamalizika na huduma zetu zitazidi kuimarika", amesema Mhandisi Matindi.
ATCL iliyoanzishwa mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wameingia mkataba wa huduma hiyo ya chumba cha daraja la juu la abiria wa biashara na VIA Aviation kwa miaka 2 na wapo mbioni kuanzisha huduma hiyo uwanja wa ndege wa Dodoma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.