RC MTANDA AWAAGIZA JIJI LA MWANZA KUMPA KAZI MKANDARASI ATAKAYEWEZA KUJENGA SOKO LA MCHAFU KUOGA USIKU NA MCHANA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Halmashauri ya jiji la Mwanza kuhakikisha wanampata Mkandarasi atakayefanya kazi usiku na mchana katika mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo la mchafukuoga ili lijengwe kwa kasi.
Amesema hayo leo Juni 03, 2024 wakati akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa huduma kwenye soko hilo lililopo kata ya Igogo na akabainisha kuwa ndani ya miezi sita wananchi watapata soko la kisasa lenye miundombinu ya Maji, Vyoo na nishati ya Umeme.
Amesema, ni lazima Halmashauri ihakikishe inalinda fedha zinazotolewa na Mhe. Rais kwa ajili ya ujenzi wa miradi na kwamba yeye kama msimamizi hatokubali kuona fedha za umma zikichezewa na watu wachache kwa kufanya ubadhirifu na atakayethubutu atamchulia hatua za kisheria.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itasaidi kuweka utaratibu wa kuwaunganisha wafanyabiashara wa Kanda ya ziwa ili kulifanya Soko hilo kuwa kitovu cha Uuzaji wa Mitumba ya nguo na kwamba hali hiyo itasaidia hata kuleta watalii kwenye soko hilo.
Hatahivyo, amezitaka Mamlaka zinazohusika na maji yaani MWAUWASA, TANESCO-Umeme, TARURA kwa ajili ya barabara pamoja na Halmashauri kuboresha huduma zote zinazowahusu ili wafanyabiashara hao wapate ridhiki kwenye eneo linalofaa na wasihatarishe afya zao.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Nyamagana alibainisha historia ya uwepo wa wafanyabishara hao kuwa ni kutokana na kupangwa kutoka uuzaji holela waliokua wakishiriki siku za nyuma kwa kuuza nguo mjini kwenye hifadhi ya barabara.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza Peter Lehhete amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa siku za karibuni atapatikana Mkandarasi wa ujenzi wa Soko hilo kwani tayari Halmashauri ipo kwenye taratibu za manunuzi na kwamba wametenga shilingi Bilioni 7 kujenga soko la Kisasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.