RC MTANDA AWAKARIMU MADIWANI KUTOKA ARUSHA JIJI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo septemba 17, 2024 amewatembelea Wahe. Madiwani, Wataalamu na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha waliowasili Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi na kujifunza mambo mbalimbali.
Mhe. Mtanda amekutana na Wahe. Madiwani hao katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na kuwakaribisha Mwanza kisha kuwataka kutembelea maeneo mbalimbali ya kiutalii ili watakaporudi Mkoani Arusha wakayaelezee yale yote mazuri waliyokutana nayo Mkoani Mwanza.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mwanza ni Mkoa mkubwa namba mbili kwa idadi ya watu pamoja na muingiliano wa shughuli nyingi za kiuchumi hivyo kuchagua Mkoa wa Mwanza hawajakose kwani ni eneo sahihi la kujifunzia, na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Waheshimiwa hao ambao pia wengi wao anafahamiana nao kwa kuwa aliwahi kufanya nao kazi wakati alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha mwaka 2021 - 2023.
Sambamba na hayo amewataka Wahe. hao kama watapata nafasi wasisite kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Mkoa wa Mwanza ambayo serikali imetoa fedha nyingi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezeka ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza, Mikoa jirani pamoja na Nchi jirani.
Naye Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhe. Maximilin Iranqe amemshukuru Mhe. Mtanda kwa ukarimu wake na kutenga muda kuwatembelea Waheshimiwa hao licha ya kuwa na ratiba ngumu, Aidha amemuhakikishia kuwa wataenenda kama alivyowashauri na kumalizia kwa kumtaka kuendelea kushirikiana nao kwa kipindi chote watakapowepo Jijini humo.
Wahe. Madiwani pamoja na Wataalamu hao wamefika Mwanza kwa lengo la kujifunza; Usimamizi na uendeshaji wa stendi ya Nyamhongolo, Uendeshaji wa vikao kwa mfumo wa e-board, Uendeshaji wa jengo la kibiashara la Rock City Mall, Usimamizi na ukusanyaji wa leseni za biashara, kodi ya pango na ushuru wa nyumba za kulala wageni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.