Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amekipongeza Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kwa kuendelea kuandaa ziara za mafunzo zinazowawezesha washiriki wake kujifunza kwa vitendo utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Akizungumza Januari 19, 2026 wakati wa mapokezi ya Washiriki wa Kozi ya NDC Kundi la 14 waliowasili Mkoani Mwanza Mhe. Mtanda amesema ziara hizo ni muhimu katika kuwajengea uelewa mpana viongozi kuhusu juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Ameeleza kuwa Mkoa wa Mwanza unaweka mkazo katika kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia ushiriki wao kwenye shughuli rasmi za uzalishaji mali, akibainisha kuwa vijana ni kundi hatarishi endapo halitapatiwa fursa na ujuzi wa kiuchumi.

Mhe. Mtanda ameongeza kuwa uchumi wa mkoa unategemea kwa kiasi kikubwa sekta ya uvuvi kutokana na uwepo wa Ziwa Victoria, pamoja na fursa za uchumi wa buluu ikiwemo uvuvi na usafirishaji wa majini.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa kilimo cha mazao ya biashara kama pamba, dengu na mpunga katika kuinua uchumi wa wananchi wa Mwanza na kuhakikisha usalama wa chakula.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Timu ya Washiriki wa Kozi hiyo, Brigedia Jenerali Method Matunda amesema washiriki watatembelea miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Uwanja wa Ndege Mwanza, Karakana ya Songoro, TASHICO, TARIāUkiriguru na Daraja la Magufuli kama sehemu ya ziara yao ya mafunzo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.