RC MTANDA AWAPONGEZA H/ ILEMELA KWA KUOKOA MIL. 26 UJENZI WA MADARASA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kuokoa fedha takribani Milioni 26 zilizobakia katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vyumba 44 vya madarasa Idara ya elimu msingi.
Pongezi hizo amezitoa mapema leo Julai 12, 2014 alipokua katika hafla fupi ya kukabidhiwa vyumba 44 vya madarasa Wilayani Ilemela, hafla iliyofanyika katika shule ya Sekondari ya Lumala iliyopo Kata ya Ilemela, Manispaa ya Ilemela kwa kumkabidhi Mkuu huyo wa Mkoa vyumba 06 vya madarasa kuwakilisha vingine.
"Ninawapongeza kwa kuokoa fedha takribani Milioni 26, na ni msimamamo wa Serikali kwamba tunapofanya shughuli za ujenzi wa miradi ya maendeleo siyo lazima fedha zote zitumike, tunaweza kuokoa fedha na tukazitumia kwa shughuli nyingine".Mtanda
Maeneo mengine wangeweza kula fedha hizo, na madarasa haya 44 yasingekamilika na sasa tungekua tunapelekana TAKUKURU huko, kwa hiyo ninawapongeza sana kwa kuokoa fedha hizo. Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Mtanda pia ametoa rai kwa wanafunzi hao kuendelea kujiimarisha kwa kusoma kwa bidii, juhudi na maarifa kwa kuwa Serikali ya Rais Samia imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu kadhalika kuwatimizia maslahi ya walimu.
"Siku hizi kuna msemo unasema kwamba elimu ya zamani ni tofauti na ya sasa, ndio ni kweli ukitizama hata madarasa haya yanavutia yana vigae, madirisha mazuri, umeme kwa ajili ya mwanga, sasa na nyie wanafunzi someni kwa bidii",amesisitiza mkuu huyo wa mkoa.
Sambamba na hayo, Mkuu wa Mkoa pia amewataka wazazi kuweka utaratibu wa kuwa karibu na watoto wao, kwa kuwa siku za hivi karibuni kumekuwa na mmonyoko wa maadili kwa watoto hivyo amewataka kusaidia katika malezi kwa kuweka utaratibu wa kuwachunguza watoto mara baada ya kutoka shuleni.
"Unakuta mzazi ametingwa kutafuta maisha wanawatekeleza watoto kwa kuwaacha wajilee wenyewe, halafu mwisho wa siku wanakuja kushtuka wanakuta tayari watoto wameshaharibika na hizo fedha zenyewe hujapata kwa hiyo kuweni makini". Mkuu wa Mkoa akisisitiza malezi bora.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ilipokea jumla ya shilingi 1,417,100,000,000.00 kati ya shilingi 2,261,000,000.00 iliidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya Sekondari, aidha kiasi cha Tshs. 1, 100,000,000.00 ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 44 vya madarasa, shilingi 187,500,000.00 ni ukamilishaji wa maboma 15 ya vyumba vya madarasa na seti ya meza na viti 2,750.
"Utekelezaji wa miradi hiyo umekamilika kwa 100% ambapo fedha iliyotumika ni 1,394,453,977.22 na bakaa ni shilingi 26,646,022.78". Amesema Mhe. Masalla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.