RC MTANDA AWASIHI TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA KAMATI ZA MAADILI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama Mkoa Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama nchini kutoa ushirikiano wa dhati ili kuimarisha Kamati za Maadili katika ngazi zote.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo Mei 13, 2024 wakati akitoa neno la ufunguzi katika mafunzo ya wajumbe wa Kamati za Maadili kwa Maafisa wa Mahakama Mkoani Mwanza yatakayodumu kwa siku mbili.
"Tume ya Utumishi wa Mahakama tunaisikia, tunaomba ushirikiano wenu wa dhati ili tuwe na uelewa wa pamoja katika shughuli za kila siku pamoja na kuimarisha Kamati za Maadili za Wilaya na hata ngazi ya Mkoa." Mhe. Mtanda.
Aidha, ametoa wito kwa taasisi hiyo kuhuisha mfumo wa utendaji wa Kamati za maadili ili kuzipa uhai kwa kuzingatia ratiba za shughuli zilizopangwa kwa mwaka ili kuhakikisha kunakua na vikao vya kisheria na kusaidia kusambaza uelewa wa pamoja kwa jamii.
Mtanda amesema, Kamati za Maadili zinasaidia sana kuijenga jamii kwa kutumia viongozi wa kisiasa hususani wakuu wa Wilaya ambao mara zote wamekua wakikutana na wananchi kwenye shughuli mbalimbali.
Naibu Katibu wa Tume (Maadili na Nidhamu) Alesia Mbuya amesema pamoja na mafunzo hayo Tume hiyo imekuja kuhuisha ushirikiano na kuzikumbusha Kamati za Maadili wajibu wao wanaopaswa kufuata kila wakati.
Vilevile, amebainisha mafanikio waliyopata Tume hiyo hususani kujenga uelewa kwa jamii wa masuala mbalimbali ya kimahakama na sheria na kutoa usaidizi kwenye uteuzi wa Majaji wa Mahakama kuu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.