RC MTANDA AWATAKA MAAFISA MIPANGO MIJI KUPANGA, KUPIMA NA KUMILIKISHA ARDHI KISHERIA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka Maafisa Mipango Miji kuhakikisha wanasaidia jamii kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kisheria ili kuondokana na migogoro ya ardhi nchini.
Mtanda amebainisha hayo leo Mei 30, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Mipango miji kutoka Mikoa ya Kanda ya ziwa kilichoratibiwa na Bodi ya Usajili wa wataalam wa mipango miji.
Amesema, katika kutimiza hilo ni lazima wajiepushe na rushwa na kuendelea kujifunza zaidi kuhusiana na masuala ya mipango miji ili kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutafuta suluhu ya changamoto za ardhi hususani ujenzi holela.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nchi nzima kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi kisheria ili kupata makazi bora kwa jamii na kuondokana na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ya hifadhi na ujenzi holela nchini.
Vilevile, ametoa wito kushirikisha sekta binafsi kushiriki kwenye upangaji wa makazi kwa ajili ya kutafuta fedha kupitia ubunifu wao na Serikali ikaweza kusaidiwa kupata rasilimali fedha hususani kwa kuandaa maandiko yatakayojikita kwenye mipango endelevu.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalam hao Dkt. Joel Msami amebainisha kuwa wanao mkakati wa kujenga mifumo nchi nzima kwa ajili ya kusimamia ardhi na majengo na kwamba wanaamini jambo hilo litasaidia kupunguza migogoro ya ardhi nchini.
Msajili kutoka Bodi ya Usajili wa Mipango Miji, Lucas Mwaisaka amesema bodi hiyo ya kitaaluma iliyoanzishwa mwaka 2009 na mpaka sasa imesajili wataalamu 456 pamoja na makampuni kadhaa na kwamba wanaendelea kuyajengea uwezo makundi mbalimbali juu ya masuala ya usajili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.