“Kwa mujibu wa ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2018 imeainishwa kuwa, tusipochukua hatua stahiki, ifikapo mwaka 2050 watu zaidi ya milioni 10 watafariki dunia kila mwaka kutokana na magonjwa yatokanayo na vimelea ambavyo vimekua sugu.”.

Ni Rai ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda aliyoitoa leo Novemba 26, 2025 kwa Wateknolojia Dawa na Wateknolojia Dawa Wasaidizi Tanzania (TAPHATA) alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa 26 wa Chama hicho.

Mkuu wa Mkoa amesema kama wataaluma wa Famasi wana jukumu la kuchukua hatua sasa katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

“Hakikisheni mnatoa elimu sahihi kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa kuwa ninyi ndio kada ya Afya inayohusika zaidi”.

Aidha Mhe. Mtanda ametoa wito kwa Mamlaka na Nabaraza yanayosimamia huduma za dawa na tiba kuhakikisha maduka yote ya dawa yanasajiliwa na kukaguliwa mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vituo vyote vya Afya vya umma na binafsi vinavyotunza dawa, vinakua na mtaalamu stahiki wa dawa kwa kuzingatia ikama ya mahali husika.

Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amesema Changamoto mbalimbali bado zipo, ikiwemo upungufu wa ajira, maslahi katika sekta binafsi, na changamoto za usimamizi wa maduka ya
dawa.
“Nitoe wito kwa Baraza la Famasi na Ofisi ya Mfamasia Mkuu wa Serikali kushirikiana kwa karibu na Chama chenu kusikiliza na kushughulikia changamoto hizi ili taaluma hii iwe na nguvu zaidi na tija kubwa kwa Taifa”.

Aidha Mhe. Mtanda amesema serikali imeendelea kuajiri watalam katika sekta hiyo na kwa mwaka huu serikali kupitia utumishi wameshatangaza ajira zipatazo 10,280 na wateknolojia Dawa wakiwemo.

Nitoe wito wasimamizi wa kada hii kupeleka mapendekezo wizarani ili kuona namna bora ya kuongeza ajira kwa wanataaluma wenu kadri inavyofaa mkiainisha pia maeneo ambayo yana ulazima wa kuwepo kwa wanataaluma kama ilivyosemwa kwenye risala yao. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.