Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka viongozi wa dini kushiriki kikamilifu katika malezi ya jamii kwa kushirikiana na Serikali, akisisitiza kuwa pande zote mbili ni wachungaji wa watu tofauti ikiwa ni majukumu na maeneo ya utendaji.

Akizungumza leo Desemba 18, 2025, wakati wa kikao na viongozi na wachungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria (DMZV), Mhe. Mtanda amesema wananchi wanaohudumiwa na Serikali ni hao hao wanaohudumiwa na viongozi wa dini.

“Watu ni wale wale isipokuwa kanisani mnawaita waumini, wanapotoka nje kwetu sisi tunawaita wananchi, na wanapokuwa sokoni huitwa wateja au wanunuzi, hivyo hakuna sababu ya kila upande kujitenga katika kuwalea kimaadili”.

Mhe. Mtanda amewataka viongozi wa dini kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa ili waumini washibe neno la Mungu na kujiepusha na vitendo vinavyokiuka maadili, sheria, kanuni, taratibu pamoja na tamaduni za Watanzania.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, ushirikiano kati ya Serikali na taasisi za dini, pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi kama nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa amewahimiza viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na viongozi wake, akisema maombi ni nyenzo muhimu katika kujenga amani, mshikamano na masikilizano kwa ustawi wa nchi.

“Kwanza kabisa, nawasihi muombe dua, msali na kumshukuru Mungu kwa ajili ya watu wote, kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema”. Amehitimisha Mkuu wa Mkoa kwa kusoma 1 Timotheo 2:1

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa KKKT, Askofu Oscar Itael Lema wa KKKT (DMZV) Mwanza amesema kanisa linaunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga jamii yenye maadili na amani.

Amesema kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuwalea waumini kiroho na kimaadili, na kuhakikisha linakuwa chachu ya amani, umoja na mshikamano katika jamii.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.