Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wazazi na wadau mkoani humo kuendelea kuchangia maendeleo ya elimu nchini hususani ujenzi wa miundombinu ya elimu kama madarasa.
Amesema hayo jioni ya leo katika shule ya awali na msingi Lake Victoria jijini Mwanza alipohudhuria hafla fupi ya kumpongeza mwanafunzi wa darasa la saba aitwaye Nursan Francis aliyeshika nafasi ya kwanza katika mitihani ya utamilifu ya darasa la saba kwa mikoa 6 ya kanda hiyo.
Akiwashukuru wadau waliochangia ujenzi wa ukumbi wa kisasa kwenye shule hiyo Mhe. Mtanda amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita imetoa zaidi ya Tshs. Bilioni 196 kuboresha miundombinu Mkoani humo hivyo wamefanya jambo jema na akatoa wito kwa wengine kuchangia.
“Mzazi hata kama utakua unatoa fedha tele za mtoto kusoma na kuinjoi bila kuwa naye karibu haisaidii maana mtoto wako atakosa msingi wa malezi bora na maadili kwani hajaishi na kuchukua tabia zako, hivyo nawaomba tutenge muda wa kukaa nao katika kipindi cha balehe.” Mhe. Mtanda akisisitiza kuhusu malezi.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. Saraphina Peter amesema hafla hiyo ya kumpongeza Nusran Francis imeandaliwa kutokana na kufanya kwake vizuri kwenye mitihani ya utamilifu darasa la saba kanda ya ziwa 2025 inayojumuisha mikoa sita kwani ameshika nafasi ya kwanza kwa kupata alama 296 kati ya 300.
Aidha, amebainisha kuwa pamoja na ufaulu huo wa mtoto Nursan, shule hiyo hiyo pia umepata ufaulu mkubwa sana kwani katika wanafunzi 86 waliosajiriwa na 85 wakiwa wamefanya mtihani wamepata wastani wa 39 kati ya alama 50 ambayo ni daraja B kasoro alama mbili tu wangekua na A.
Uongozi wa shule hiyo umempatia zawadi ya Kompyuta mpakato mpya mtoto Nursan pamoja na nafasi ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne bila kulipia ada pamoja na mwanafunzi mmoja atakayepelekwa kwenye shule hiyo na Mkuu wa Mkoa atapata elimu bure.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.