RC MTANDA AWATAKA WAFANYABIASHARA KUWA NA SUBIRA WAKATI SOKO KUU LA MJINI KATI LIKITARAJIWA KUTOA HUDUMA HIVI KARIBUNI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wafanyabiashara mjini Mwanza kuwa wavumilivu na kuendelea na biashara zao kwenye eneo walilopangwa kwani ujenzi wa Soko Kuu la Jijini humo lipo mbioni kukamilishwa.
Ametoa wito huo leo Juni 03, 2024 wakati akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Mbugani waliohamishiwa hapo kwa muda mfupi kupisha ujenzi wa Soko kuu la mjini kati linalotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 23.
"Serikali imeridhia kummalizia mkandarasi shs bilioni 3 zilizobaki hivyo tuna imani kasi ya umaliziaji sasa itakwenda vizuri na wafanyabiashara mtaanza kutoa huduma kwenye mazingira bora na ya kisasa," amesema Mkuu wa Mkoa.
Mtanda amesema, kwa sasa ni hasara kuwekeza kwenye soko la muda kwani eneo hilo ni la muda mfupi na kwamba nguvu kubwa imeelekezwa kwenye ujenzi wa soko la Mjini Kati ambalo ujenzi wake umeshafikia zaidi ya asilimia 90.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema mara baada ya soko kuu kukamilika wafanyabiashara wa Mbugani watapewa kipaumbele kuingia rasmi soko jipya kama walivyoahidiwa awali na Serikali.
Aidha, ametumia jukwaa hilo kuwashukuru Baraza la Kiislam Nchini (BAKWATA) kupitia Msikiti mkuu wa Mwanza kwa kutoa eneo hilo linalotumiwa kwa muda kwa sasa wakati ujenzi wa soko la kuu ukiendelea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.