RC MTANDA AWATAKA WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA WILAYA KUSIMAMIA UPATIKANAJI WA DAWA KWA KARIBU
kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi juu ya wizi wa dawa, kununua dawa nyingi na hatimaye kuchina na kusababisha hasara kwa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka na kuwaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Kanda ya Mwanza kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa dawa kwa karibu.
Mhe. Mtanda ametoa kauli hiyo wakati akihutubia katika mkutano wa mwaka na wadau wa afya kanda ya Mwanza uliofanyika leo Juni 26, 2024 mkoani humo,Mhe. Mtanda amewataka waganga wakuu wa wilaya na Wafamasia wa mikoa kukagua na kufuatilia matumizi ya bidhaa za afya katika kila ngazi ili kudhibiti mianya ya upotevu wa bidhaa hizo.
"Ni mategemeo yangu kuwa baada ya mkutano huu, wote tutaondoka na uelewa wa pamoja na maazimio ambayo utekelezaji wake utaboresha upatikanaji wa bidhaa za afya pamoja na kuboresha huduma za afya maeneo yetu ya kazi".
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewakumbusha wadau wa MSD kupitia Wizara ya afya, kufanya maoteo ya bidhaa za afya kwa usahihi, weledi na kwa wakati, hii itawezesha MSD kuwa na takwimu sahihi katika bidhaa za afya kuagiza kutoka kwa wazalishaji na washitiri hivyo kuboresha upatikanaji wa bidhaa hizo.
Kadhalika Mhe. Mtanda amewataka waganga wakuu wa wilaya na wafamasia kusimamia ukusanyaji wa mapato katika vituo vya kutolea afya ili vituo hivyo viweze kulipa madeni yaliyopo MSD kwa wakati mara baada ya kupokea shehena ya bidhaa na kuepusha madeni yasiyo ya lazima.
"Ninawakumbusha pia mna jukumu la kuvisimamia vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yenu ili viweze kukusanya mapato ya kutosha yanayotokana na uchangiaji wa huduma za afya".Mkuu wa Mkoa
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya dawa (MSD) Bw. Victor Sungusia amesema mikutano ya mwaka na wadau wa afya ni muhimu sana kwa pande zote mbili yaani MSD yenyewe na viongozi wa sekta ya afya ngazi ya Mkoa na Wilaya, kwa sababu wakati wa kikao hicho kuna mambo yatawasilishwa na kujadiliwa ambayo ni muhimu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.