RC MTANDA AWATAKA WANANCHI KUTUMIA ILEMELA NYAMA CHOMA FESTIVAL KUKUZA BIASHARA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Novemba 16, 2024 amezindua tamasha la Ilemela nyamachoma na amewataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kukuza mitaji na kipato cha biashara zao.
Amesema wananchi hawana budi kulitumia eneo hilo kujenga mahusiano mema na yenye tija kibiashara na liwe eneo mashughuli kwa nyama choma, vyakula vingine na vinywaji na kupumzika ambapo litasaidia kukuza utalii.
"Huu ni mwanzo, matarajio ni kuboresha zaidi eneo hili na siku za usoni tutakua na nyama choma, muziki mubashara na pombe na Nyamhongolo itakua maarufu kwa shughuli hizi na wageni wakifika Mwanza watajua eneo rasmi ni hapa."
Aidha, amebainisha kuwa uwepo wa shughuli rasmi wakati wote kwenye eneo hilo utasaidia pia kujenga jamii ya Mwanza kimaadili kwa kulitumia eneo hilo kujengana katika makundi mbalimbali ya kijasiriamali.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bi. Ummy Wayayu amesema kwa kushirikiana na wadau wataendelea kuboresha eneo hilo na kwamba uwepo wa Nyama choma utasaidia wananchi kupata sehemu ya kupoteza mawazo.
Naye, Mbunge wa Ilemela Mhe. Dkt. Angelina Mabula ametumia wasaa huo kumpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwa ubunifu ambao amebainisha kuwa tamasha hilo litasaidia kukuza mapato ya halmashauri.
Aidha miongoni mwa maoni mengi ya wadau wa nyama choma wameomba kuboreshewa miundombinu ya eneo hilo ili liweze kuwa bora zaidi na vyombo vya habari kuendelea kulitangaza tamasha hilo ili lizidi kuwa kubwa zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.