RC MTANDA AWATAKA WANANCHI KUWAENZI MASHUJAA KWA KUWA WAZALENDO NA WAADILIFU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi Mkoani humo kuwaenzi mashujaa walioipigania nchi wakati wa Uhuru kwa kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kuwa wazalendo kwa Taifa.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo mapema leo 25 Julai 26, 2024 wakati akitoa salamu za Serikali na hotuba kwa wananchi katika maadhimisho ya siku ya Mashujaa, hafla iliyofanyika katika viwanja vya mzunguko wa ziro ziro jijini Mwanza.
"Tunapaswa kuwaenzi mashujaa kwa kuachana na matendo ya kujihusisha na rushwa, kupambana na dawa za kulevya na ujangili wa wanyamapori, kufanya kazi kwa bidii pamoja na kuwa wazalendo kwa ujumla kwa Taifa." Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda amesema wananchi wana kila sababu ya kuwakumbuka mashujaa waliopoteza maisha wakiwa wanatetea na kupigania uhuru wa Tanzania na akatoa wito kwao kuwaombea dua na sala maalum.
"Historia ya Tanzania haiwezi kukamilika bila kuwataja mashujaa waliotumia mbinu na silaha za asili dhidi ya wakoloni waliotumia silaha wakati wa kulikomboa Taifa hili, twendeni tukapande mbegu ya utaifa, upendo, mshikamano ili kulinda mipaka na rasilimali za nchi yetu." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, ametoa wito kwa jamii kujiandaa na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura zoezi litakaloanza Agosti 21, 2024 pamoja na kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa mwishoni mwa mwaka huu ili kuwapata viongozi wa Serikali ngazi ya mitaa, vijiji na Vitongoji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.