RC MTANDA AWATAKA WANUFAIKA WA MRADI WA VIZIMBA KUWEKA UMAKINI KATIKA UWEKEZAJI HUO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka vijana waliokopeshwa vizimba vya kufugia samaki Kanda ya Ziwa Viktoria hususani Mkoa wa Mwanza kuhakikisha wanaweka umakini wa kutosha katika usimamizi wa uwekezaji huo ili uwaletee manufaa.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo Agosti 07, 2024 alipotembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo uliotolewa kwa mkopo bila riba kupitia benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) kwa makundi maalum ya wanawake, walemavu na Vijana katika mtaa wa Kisoko uliopo Wilayani Nyamagana.
Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wanufaika hao kuzingatia pia utunzanji wa kumbukumbu kwa kipindi chote wawapo shambani hapo, aidha ameutaka uongozi wa mahali hapo kuhakikisha wanakuwa na daftari maalumu la wageni ambalo pia watalitumia kuandika maoni yao ili wakija viongozi na wageni mbalimbali watumie daftari hilo katika kutazama na kuona ni kwa namna gani wanaweza wakatatua changamoto au kero zilizoainishwa katika daftari hilo.
"Mali bila daftari huisha bila habari, ni lazima muwe na daftari la wageni hata kama anakuja DC anakuta mmendika changamoto ya barabara basi yeye atajua ni namna gani ataliwasilisha suala hilo kwa mamlaka husika na changamoto yenu inakua imepata tiba". Mhe. Mtanda.
Kadhalika Mhe. Mtanda amewataka wanufaika hao kuweka umakini wa hali ya juu kwa kuwa na usimamizi bora wa vizimba hivyo kwa kuwa Serikali ya Rais Samia imedhamiria kwa dhati kuwasaidia wananchi wake kujikwamua na umaskini kwa kuwapatia wanufaika hao zaidi ya shilingi bilioni 4 katika uwekezaji huo wa ufugaji wa samaki wa vizimba.
"Msifanye mambo kwa kutania tania, kama mmedhamiria kufanya uwekezaji hapa ziwani basi acheni ubabaishaji kuweni makini katika kusimamia, msipofanya hivyo nyie wapo wageni watakaokuja kuitumia fursa hii vizuri. Ameongeza Mkuu huyo wa Mkoa.
Mkoa wa Mwanza umebahatika kupata wanufaika wengi ambao ni 69 (Vikundi, ushirika na watu binafsi wenye wanufaika 1305) pamoja na vizimba 255 vya mkopo usio na riba, ambapo kwa eneo la Kisoko pekee vimesanikishwa vizimba 112 na kuna jumla wanufaika 392 kwa awamu ya kwanza na ya pili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.