RC MTANDA AZINDUA RASMI BODI YA USHAURI HOSPITALI YA SEKOU TOURE,AHIMIZA MABORESHO
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe: Christopher Ngubiagai amezindua rasmi Bodi ya ushauri ya Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Seko Toure na kutoa rai kwa wajumbe wa bodi hiyo wazingatie mikakati na maamuzi yanayolenga kuboresha huduma, kuwakilisha maslahi ya wananchi Kwa uwazi na uadilifu na kuhakikisha rasilimali za Hospitali zinatumika Kwa njia bora.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza comrade Ngubiagai amebainisha ni wajibu wa Bodi hiyo ya Afya kuhamasisha uwekezaji katika mifumo ya kidigitali, kuanzisha programu ya mafunzo Kwa watoa huduma,kukuza ushirikiano na wadau wa sekta ya afya na Kuboresha ufanisi wa kuongeza mapato ya Hospitali.
"Tumeona juhudi za Serikali namna inavyoboresha sekta ya afya,miradi mingi imeletwa mkoani Mwanza na hospitali hii sasa inatoa huduma nyingi za kibingwa,tunapaswa kuunga mkono juhudi hizi kwa kuleta ubunifu zaidi wenye tija,"amesisitiza mkuu huyo wa wilaya wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa bodi hiyo ya ushauri.
Ameongeza kuwa kupitia Bodi ya ushauri yenye wataalam wa sekta ya afya ni wajibu wao kuhakikisha wanaleta mageuzi chanya kwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali, ufuatiliaji, uwajibikaji wa watendaji na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure Bw. Alhaji Sibtain Meghjee amesema uzinduzi wa Bodi hiyo utakuwa na kielelezo tosha cha kuimarisha na kuboresha huduma na wananchi watapata huduma bora na kwa wakati
Katika hatua nyingine Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekoutoure Dkt.Bahati Msaki amemshukuru mgeni rasmi kwa kuzindua Bodi ya Ushauri ya Hospitali na kuahidi kutoa ushirikiano kati ya bodi hiyo na watumishi wa Hospitali ya Sekoutoure ili kuendelea kuboresha huduma za afya
Sanjali na uzinduzi huo pia Mkuu huyo wa wilaya na wajumbe wa bodi walifanya ziara na kukagua huduma mbalimbali zitolewazo Hospitalini hapo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.