RC MTANDA AZINDUA RASMI KAMATI YA USHAURI WA KISHERIA YA MKOA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameizindua rasmi kamati ya ushauri wa kisheria ngazi ya Mkoa na kutoa wito kwa wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa weledi.
Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo leo kwenye viwanja vya Ofisi ya mkuu wa mkoa, Mtanda amesema kuwa kamati hiyo itasaidia wananchi kwa kupata huduma ya kisheria bila malipo.
"Nawaomba sana wajumbe wa kamati hii iliyojaa wataalamu fanyeni kazi kwa weledi, tutawatathmini kuona mnavyowahudumia wananchi", amesisitiza mkuu wa mkoa wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo.
Aidha, Mhe. Mtanda amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mpango huo wa kuwasogezea karibu wananchi huduma hiyo ya kisheria huku migogoro mingi ya ardhi ikiongoza.
"Ofisi yangu kila siku ya Jumanne tunasikiliza kero za wananchi, idadi kubwa ya wananchi wanaofika wanasumbuliwa na migogoro ya ardhi, sasa kamati hii naomba mtambue kuwa sitapenda kuona wananchi wanatoa malalamiko haya kwa viongozi wa juu", ameongeza.
Ametoa pia maelekezo kwa wakuu wote wa Wilaya mkoani Mwanza kwenda kuziunda kamati hizo ngazi za wilaya ambazo zitashirikiana na kamati ya Mkoa kutatua kero za wananchi.
Akitoa taarifa fupi kuhusiana na kamati hiyo, mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Neema Ringo amesema zaidi ya kesi 500 kwa mwaka wanazipokea za wananchi kuishtaki Serikali, hivyo kuundwa kwa kamati hiyo itapunguza kesi hizo.
Mpango huo ulizinduliwa rasmi Machi 21, 2024 na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.