Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amezitaka Halmashauri Mkoani humo kuhakikisha wanapeleka fedha za lishe kwenye shule kwa ajili ya kununua virutubisho na chakula dawa cha watoto kwa mujibu wa bajeti zao .
Ametoa wito huo mapema leo agosti 22, 2025 wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Juni 2024/25 kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema Wakurugenzi ni lazima watimize wajibu wa kutenga bajeti na kupeleka fedha za masuala ya lishe shuleni kwa ajili ya kutekeleza afua za lishe kwa watoto ili kujenga taifa lisilo na utapia mlo na udumavu.
Aidha, amezipongeza Halmashauri za Buchosa, Ilemela, Kwimba, na Sengerema kwa kupeleka fedha hizo na kupelekea mkoa kuwa na wastani wa aslimia 92 katika kishiria hicho.
Kadhalika, amezitaka Halmashauri zilizofanya chini ya ufanisi wa wastani huo vizuri na kukwamisha kufikia malengo kuongeza juhudi kuhakikisha hawaurudishi nyuma mkoa kwenye masuala ya lishe.
Katika kufanikisha afua hiyo, Mhe. Mtanda amewataka idara ya Elimu kuhamasisha wazazi na walezi kutoa michango kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa chakula kwa watoto shuleni na amezitaka shule zenye mashamba kulima mazao ya lishe kwa ajili ya kuongeza virutubisho kwenye chakula wanachopatiwa watoto.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwataka viongozi na watendaji kwenda kuhamasisha wananchi waweze kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba 2025 kwa amani na utulivu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.