RC MTANDA : TUTAFANIKIWA KUKABILIANA NA DAWA ZA KULEVYA ENDAPO USHIRIKIANO UTAIMARISHWA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema tutafanikiwa kukabiliana na kuondokana na tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwa tutashirikiana wote kwa pamoja yaani Serikali, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na jamii kiujumla kuijenga jamii isiyotumia dawa za kulevya.
Mhe. Mtanda ametoa rai hiyo wakati akiwahutubia wanachi waliohudhuria katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya leo Juni28, 2024 katika uwanja wa Nyamagana uliopo Jijini Mwanza.
"Ninaomba tuungane wote katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, tusikubali dawa za kulevya ziharibu jamii yetu, Kwa pamoja tunaweza kulikabili janga hili".Mkuu wa Mkoa
Aidha Mkuu wa Mkoa ameendelea kusema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais shupavu Dkt. Samia imedhamiria kwa dhati kupambana na tatizo la dawa za kulevya kwa nguvu zote, hali hiyo inatokana na utashi wa kisiasa ambapo amesema Serikali inatekeleza kwa vitendo ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2022/2025 ibara ya 245 (a)-(e).
"Ilani imeielekeza Serikali kuchukua hatua za kupambana na uzalishaji, usambazaji, uuzaji, na utumiaji wa dawa za kulevya".Mtanda
Mkuu huyo wa Mkoa amesema maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika kuanzia leo Juni 28- 30 2024 lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Watanzania kwa pamoja kutafakari, kutambua, na kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo jamii kupewa elimu zaidi juu ya athari za dawa za kulevya na namna tiba zinavyotolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya.
Maadhimisho ya mwaka 2024 yanaongozwa na kauli mbiu isemayo "Wekeza kwenye Kinga na Tiba Kudhibiti Dawa za Kulevya" ambapo inasisitiza elimu kwa jamii ili iweze kufahamu madhara ya dawa za kulevya na kushirikisha jamii katika kutatua changamoyo zinazotokana na dawa za kulevya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.