Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe,Mhandisi Robert Gabriel amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri Mkoani humo kuandaa mpango kazi wa utoaji wa Elimu na kusimamia urejeshwaji wa mikopo itolewayo kwa makundi ya Vijana,Wanawake na Walemavu.
Akizungumza na vyombo vya Habari Mkoani Mwanza,Mhandisi Gabriel amesema mbali na utoaji huo wa Elimu
pia amesimamisha zoezi la utoaji Mikopo kuanzia leo Aprili 25 2022 ili hatua sahihi za urejeshwaji huo ufanyike.
"Unakuta Kikundi kinapishana na andiko la Mkopo na kile wanachofanya baada ya kupata fedha matokeo yake wanayumba na mwisho wanashindwa kurejesha" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
"Hatuwezi kuendelea na utoaji wa Mikopo wakati kuna deni la zaidi ya Bilioni 4 ambalo limechangiwa na ukiukwaji wa utoaji wa Mikopo hii" amesisitiza Mkuu wa Mkoa Mhandisi Gabriel.
Amesema zimetolewa fedha za mikopo jumla ya shs Bilioni nane na bado zaidi ya Bilioni 4 hazijarejeshwa lazima liwepo jambo la kufanya kuhakikisha fedha hizi zinarudi kwa kuwashirikisha TAKUKURU pia.
Mhandisi Gabriel amesema uchunguzi wa awali umeonesha ama kwa kutofahamu au ufujaji bado watoaji na wanufaika wamekiuka taratibu za Mikopo hii.
Amesema hiyo Mikopo haijatolewa kama zawadi imewalenga Makundi maalum ya Vijana,Wanawake na Walemavu kukabiliana na changamoto za ajira hivyo ni lazima zirejeshwe ili na wengine wanufaike nazo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.