Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba leo Desemba 29, 2025, amefanya ziara maalum ya kikazi Wilaya ya Sengerema kwa lengo la kukagua vituo vya afya na zahanati zinazoendelea na ujenzi pamoja na zile zinazotoa huduma kwa jamii ili kujiridhisha na utendaji kazi na ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi.

Dkt. Lebba ametembelea jumla ya vituo vitano ambavyo ni Zahanati ya Tabaruka, Ngoma B na Nyalwambu pamoja na Vituo vya Afya vya Kaomolo na Kamanga, ambapo amekagua maendeleo ya ujenzi, upatikanaji wa huduma na mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi.

Akiwa katika ziara hiyo, amewataka mafundi na wasimamizi wa miradi kuongeza kasi ya ujenzi ili vituo hivyo vikamilike kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.

Hata hivyo, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha vituo ambavyo bado havijakamilika vinakamilishwa kwa kuzingatia muda uliopangwa.

Aidha, Dkt. Lebba amemshukuru Mhe. Rais Dr. Samia suluhu Hassan kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya hususani katika miundombinu, vifaa tiba, bidhaa za afya pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watumishi wa afya, jambo linalochangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na hii ni utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ndani ya siku 100 kwa kuhakikisha vituo vya huduma za afya vinakamilika na kuanza kutoa huduma bora.

“Uwekezaji mkubwa umefanyika upande wa miundombinu, vifaa tiba, bidhaa za afya kwa ujumla pamoja na watumishi, na ndio maana tunaweza kuwagawa katika maeneo mbalimbali ya utendaji kazi,” amesema Dkt. Lebba.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Dkt. Darison Andrew, amesema kuwa upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 95.2%, wahudumu wa afya wanapatikana na huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, huku baadhi ya vituo vikiendelea kufanyiwa maboresho.

Hata hivyo amepongeza ujio wa Mganga Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye viwango vya juu.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.