Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza leo tarehe Agosti 5, 2025, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watoto Wachanga (Neonatal Care Unit - NCU) katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba.
Akizungumza katika ziara hiyo Dkt. Lebba amesema kuwa ujenzi wa kitengo hicho ni hatua mahsusi katika kukabiliana na changamoto ya vifo vya watoto njiti ambao wengi wanapoteza maisha kutokana na ukosefu wa huduma maalum, vifaa tiba vya kisasa pamoja na uhaba wa wahudumu waliobobea katika afya ya watoto wachanga.
“Ujenzi wa Kitengo cha Huduma kwa Watoto Wachanga ni hatua muhimu sana katika kupambana na changamoto ya vifo vya watoto njiti,” amesisitiza Dkt. Jesca.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi madhubuti katika kuimarisha sekta ya afya, hasa katika maeneo yanayolenga kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Naye, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Doris Mollel Foundation Bw. Antonio Luis ameishukuru Wilaya hiyo kwa kuipokea taasisi hiyo na kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto ya kuokoa maisha ya watoto wachanga, hasa wale wanaozaliwa kabla ya muda.
Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi ya Doris Mollel Foundation ukiwa na lengo la kuongeza uwezo wa kutoa huduma bora kwa watoto wachanga, hususani wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.