Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba ametoa wito kwa wadau wa Malezi mkoani humo hususani wajumbe wa mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia kuwa wabunifu katika kuhakikisha wanafikisha elimu hiyo kwa jamii kwa ajili ya ustawi wa jamii.
Ametoa wito huo mapema leo Agosti 19, 2025 wakati akifungua mkutano wa maandalizi ya kikao cha malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kitakachofanyika mapema mwezi Septemba 2025 chini ya uongozi wa Katibu Tawala wa Mkoa.
Amewataka wadau hao kuhakikisha wanatumia fursa ya ratiba ya wizara ya mwezi huo wa uelimishaji unaoambatana na wiki ya ustawi wa jamii kwenda kutoa elimu kwenye jamii kwa kutumia mbinu mbalimbali kama redioni na mikusanyiko vijijini kuhusiana na malezi na ukatili wa kijinsia kabla ya kuchukua sheria kwa wakaidi.
Amesema serikali imeweka afua tano kuhakikisha makuzi, malezi na maendeleo ya mtoto yanakua na ustawi na kwamba programu mbalimbali zinazosawili afua hizo yanapaswa kuzingatiwa kwa gharama yoyote ili mwisho wa siku jamii iwe salama.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwashukuru wadau wote pamoja na kumpongeza Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa pamoja na wasaidizi wake kwa uchapakazi kwani Mwanza imepiga hatua kubwa katika kuelimisha na kupunguza matendo ya ukatili kutokana na juhudi zao za kuhakikisha elimu ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto inawafikia wananchi.
Akitoa salamu za Wizara ya maendeleo ya Jamii Idara ya Mtoto bi. Mery Shila amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na mikoa wanahakikisha mtoto kuanzia mwaka mmoja hadi minane analindwa na jamii nzima na ndio maana wanasukuma afua mbalimbali za malezi.
Aidha, amebainisha kuwa viongozi wa dini kote nchini wamekua kiungo kikubwa kwenye malezi ya watoto kwa kutoa malenzi na mafundisho ya kiroho katika kuhakikisha wanakua na tabia njema ili ikiwezekana madawati ya jinsia yakose mashauri ya ukatili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.