Umoja wa wanawake wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Mwanza –SAUT wameaswa kusajiri kikundi hicho kisheria ili waweze kufaidika na fursa mbalimbali za kiuchumi katika kuelekea uchumi wa viwanda na malengo ya maendeleo ya Dunia ya Milenia.“Millennium Development Goals”.
Haya yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa M10 Chuoni hapo, akiwa ni mgeni Rasmi katika Jumuiya ya Chuo hicho,Kampasi ya Malimbe Jijini Mwanza ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ya maadhimisho hayo kitaifa ni KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA,TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI.
Akihutubia katika maadhimisho hayo Mhe. Mongella amewataka washiriki wote wa maadhimisho hayo kujiuliza maswali yenye kuleta dhana nzima ya siku ya wanawake, “Nini maana ya siku hii, ilianzishwa na nani, ilianzishwa kwa sababu zipi,Je wadau wa maendeleo hususani Taasisi za Elimu ya juu kama SAUT kupitia tafiti mbalimbali zinasaidiaje jamii ya akina mama, na zinamuhusishaje mwanamke aliyeko kijijini kuijua dhana nzima ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”.Alisema Mhe.Mongella.
Mhe. Mongella amesisitiza kuwa zaidi ya kusherekea mafanikio na jitihada za kuleta usawa wa kijinsia katika familia, katika jamii, na katika taasisi zetu tunao wajibu wa kutumia muda kutafuta fursa na kutafuta majibu ya changamoto mbalimbali katika jamii ili kuendelea kubomoa ukuta unaokwamisha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Aidha, amefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya Chuo kikuu cha SAUT na Shule za Sekondari ambazo ni majirani na Chuo hicho katika Mkoa wa Mwanza hali inayotia hamasa hususani kwa vijana walioko Sekondari kuuona umuhimu wa kuifikia elimu ya juu, ambapo Sera ya Awamu ya tano ni “kuelekea uchumi wa viwanda” na vijana ndio tegemeo la nguvu kazi ya uzalishaji kupitia viwanda vyetu tunavyoviandaa hivyo ameahidi Serikali ya Mkoa kuendelea kutoa ushirikiano katika suala zima la ulinzi na usalama,na shughuli nyinginezo za kimaendeleo.
Mhe.Mongella ameawahidi kuwashirikisha hususani wanawake katika fursa zitakazijitokeza katika ofisi yake na wadau wa maendeleo ya wanawake Kitaifa na Kimataifa,pia amewataka kuwa wabunifu wa miradi na shughuli zinazowalenga wanawake vijijini kwa kuwaelimisha na kuwashirikisha kupitia dhana ya usawa kwa mpango wa huduma kwa jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.