Katibu tawala Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio ameongoza kikao cha sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi na Sera ya Taifa Ya Nyumba kwa niaba ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa Mhe. John Mongella ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho.
Akiongea katika kikao hicho chenye lengo la kujadili sera ya mapendekezo ya makazi na sera ya Taifa ya nyumba Kadio amebainisha kuwa takwimu zinaonyesha asilimia 75% ya wakazi wanaoishi mijini wanaishi kwenye makazi holela na kwamba makazi hayo yana upungufu wa miundombinu na huduma zingine za kijamii.
"Takwimu za watafiti zinaonyesha wakazi zaidi ya asilimia 75% mijini wanaishi kwenye makazi holela au yasiyopangwa, makazi hayo yana upungufu mkubwa wa miundombinu na huduma zingine za kijamii. '' Alisema kadio.
Pia, kadio ameeleza kuwa warsha za kuwasilisha sera zilizopitiwa na wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi zitawasilishwa kila kanda na kuwa maamuzi hayo ya kuwasilisha na kupata mchango kutoka kwa wadau yanaonyesha umuhimu wa wadau katika jukumu la kuhakikisha taifa letu lina sera zinazoainisha maisha ya baadae ya watanzania.
"Maamuzi ya kuwasilisha na kupata mchango wa wadau kutoka kanda zote za wizara yanaonyesha umuhimu wa sera hizo kitaifa pamoja na nafasi muhimu ya wadau katika jukumu la kuhakikisha kuwa taifa letu lina sera zinazoainisha maisha halisi ya lengo la mategemeo ya baadae ya watanzania. "
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dkt. Phillis Nyimbi, amesema kuwa kuwepo kwa warsha ya kuwasilisha sera zinazoandaliwa ina tija katika mkoa wa Mwanza kwani amekuwa akikutana na migogoro mingi ya ardhi, vile vile na makazi ambayo ni holela.
"Kuwepo kwa warsha hii ya kuwasilisha sera zinazoandaliwa ina tija kubwa sana kwa Mkoa wa Mwanza kwani kama kiongozi nimekuwa nikikutana na migogoro mingi sana ya ardhi, na makazi mengi ambayo ni holela," Alisema Dkt. Nyimbi.
Akizungumza katika kikao hicho Muhadhiri Mwandamizi Chuo cha Ardhi Prof. Wilbard Kombe amesema kuwa kunapokuwa na makazi bora kunawasaidia watu wa kima cha chini kuzalisha kipato na kupata nafuu ya kuishi maisha yao, lakini pia kunaleta mabadiliko katika taifa na kuweza kufikia uchumi wa kati.
"Kuwepo kwa nyumba hasa kwa watu wa kima cha chini ndiyo mahali watu wanazalisha kipato na kupata nafuu ya kuishi maisha yao,"alisema Prof. Kombe.
Naye mtafiti kutoka chuo cha Ardhi, Dkt. Tatu Limbumba amebainisha kuwa asilimia kubwa ya watanzania wanaishi katika nyumba za kupanga, makazi duni kwa kuhofia kuchukuwa mikopo kutoka katika mashirika tofauti kwani hali zao za uchumi ni duni.
"Chunguzi nyingi zimebaini kuwa asilimia 50 ya binadamu tunaishi nyumba za kupanga, makazi duni, nyumba zilizojengwa na mafundi wasio na ujuzi, na changamoto kubwa ni idadi kubwa ya watanzania wanaogopa kukopa pesa au nyumba katika mashirika tofauti tofauti kuhofia hali ya uchumi waliyonayo," Alisema Dkt. Tatu.
Pamoja na hayo Kadio amewataka wadau wote wa kikao hiki kuwa watakapo ondoka wakafikishe madhumuni ya kikao hicho katika jamii na sehemu wanazofanya kazi na kusema kuwa huu ni wajibu unawahusu viongozi wote, watumishi wa umma, taasisi binafisi na za serikali, vile vile amewasihi wadau hao kushiriki kikamilifu katika kufuatilia mawasilisho ya wataalamu na kutoa hoja zinazosaidia kuboresha sera hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.