*SERIKALI IMEKUJA NA NJIA ZA KUDHIBITI UBORA NA USALAMA WA CHAKULA NA VIPODOZI*
*TBS yasaini mkataba wa mashirikiano katika utekelezaji wa kanuni ya ushirikiano na Halmashauri za Mwanza*
*Serikali yadhamilia kupanua wigo wa kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi*
*TBS Yagawa Vishikwambi kila Halmashauri kurahisisha utekelezaji wa shughuli za ukaguzi*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amesema Serikali imekuja na njia za kuhakikisha shughuli za kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi zinafanyika kwa uharaka na kwa ufanisi ili kuhakikisha bidhaa zilizopo sokoni zipo kwenye viwango vinyofaa.
Amesema hayo leo tarehe 09 Juni, 2023 wakati wa *uwekaji wa saini katika mkataba wa mashirikiano katika utekelezaji wa kanuni ya ushirikiano ya mwaka 2021 baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Jiji za Mkoa wa Mwanza.*
"Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa inakuwa na mtandao mkubwa unaoshughulikia shughuli za *udhibiti wa ubora na usalama wa chakula na vipodozi* kwa kulitekeleza hili serikali imeamua kuwatumia wakaguzi walio chini ya Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika shughuli za udhibiti wa bidhaa husika ili kulinda afya za watumiaji katika maeneo yao," amesema Ndg. Elikana.
Zoezi la uwekaji wa saini katika mkataba huo limeambatana na *ugawaji wa vishkiwambi ambavyo vitawasaidia katika utendaji kazi* kwa waratibu wa TBS waliopo katika Halmashauri ambapo Ndg. Balandya amewataka kuhakikisha vitendea kazi hivyo vinafanya kazi kwenye majukumu husika.
" Napenda ieleweke kuwa kitendea kazi hiki sio mali binafsi ya mtumishi atakayekabidhiwa bali ni mali ya Halamashauri na kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri anao wajibu wa kuhakikisha kitendea kazi kinatumika kwa majukumu kusudiwa na endapo mtumishi aliyekabidhiwa akihamishiwa ama kubadilishiwa majukumu basi aliyeteuliwa badala yake akabidhiwe ili kuendeleza majukumu ya udhibiti," ameongeza Ndg.Balandya.
Naye, Meneja wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Bi. Happy Kanyeka amesema baada ya kukasimisha majukumu hayo kwenye ngazi za Halmashauri italeta wepesi katika kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini na kuwapatia huduma kwa uharaka.
"Baada ya kukasimisha majukumu kwenye halamashauri huduma zitakwenda kufika hadi kwenye ngazi za kata kwa kuwa watumishi wa TBS tulikuwa hatuwezi kufika katika halamashauri zote lakini tukaona madalaka kukasimishwa kwenye ngazi za Halmashauri huduma zitapatikana kwa wananchi wote,"amesema Bi. Kanyeka.
" Baada ya kusaini mikataba hii na kugawa vitendea kazi katika Halamashauri zote za Mkoa wa Mwanza zitakwenda kuanza kufanya kazi rasmi kuanzia Julai 1, 2023," amesisitiza Bi. Kanyeka
*Uwekaji wa saini wa mkataba wa utekelezaji* wa kanuni husika ni mwendelezo wa mafunzo yaliyokuwa yameendeshwa hapo awali na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mnamo Septemba, 2022 kwa baadhi ya watumishi kutoka ofisi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.