Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inathamini mchango wa walimu katika ujenzi wa Taifa.

Akizungumza katika hafla ya kikao cha Watumishi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mhe. Mtanda ameeleza kuwa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, serikali imefanya maboresho makubwa katika maslahi na mazingira ya kazi ya walimu.

“Mafanikio haya yanajidhihirisha katika kuongezeka kwa ajira za walimu kila mwaka. Hivi sasa usaili unaendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi, ambapo walimu 1,168 wameajiriwa mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2021,” amesema Mhe. Mtanda.

Aidha, amebainisha kuwa serikali imeongeza juhudi katika kuboresha miundombinu ya shule, kulipa madeni ya walimu kwa wakati, na kuanzisha mifumo ya kidijitali inayorahisisha huduma kwa watumishi wa umma.

Miongoni mwa mafanikio mengine, serikali imefanikiwa kugawa zaidi ya vitabu milioni 6.1 kwa shule za msingi na sekondari, ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Kwa upande mwingine, Mhe. Mtanda amesisitiza kuwa licha ya changamoto zilizopo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha na watu kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Katika kipindi cha 2021-2025, Mkoa wa Mwanza umepokea zaidi ya shilingi 96 bilioni kwa ajili ya elimu bila malipo, ikilinganishwa na TSh. bilioni 65 zilizotolewa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2020/2021.

Mhe. Mtanda amemalizia kwa kuwataka walimu kuwa na mshikamano katika chama chao, akisema, “Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Tuwe na umoja ili kuendeleza malengo yetu ya kuboresha sekta ya elimu.”

Huu ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kuboresha sekta ya elimu na kuwaheshimu walimu, ambao ni nguzo muhimu katika maendeleo ya taifa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.