SERIKALI KUENDELEA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UWEKEZAJI
Serikali imedhamiria kuendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kwa wawekezaji kuwekeza Mkoa wa Mwanza na Tanzania kiujumla ili kuchochea maendeleo na kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda alipokuwa katika ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo katika kiwanda cha Ziwa Steel kilichopo Nyanguge Wilayani Magu.
Mkuu wa Mkoa amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji kwani Taifa likiwa na viwanda vingi inasaidia katika upatikanaji wa ajira, ukusanyi wa kodi na upatikanaji wa bidhaa kwa urahisi zitakazozalishwa kupitia wawekezaji hao.
“Kwa niaba ya Serikali ninaomba kuwapongeza Mkurugenzi na timu yako, lakini pia nitumie wasaa huu kuwakaribisha Wawekezaji katika Mkoa wetu wa Mwanza na Mwanza ni salama sana kwa uwekezaji”.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda amesema kilichomfurahisha zaidi ni kusikia kuwa kiwanda hicho kina mpango wa kuanza kutengeneza nashine za uchakataji wa dhahabu ambapo kwa ukanda huu ndio ukanda wa madini hayo.
“Mtakapoanza uzalishaji wa mashine hizo basi rai yangu ni kwamba msiwasahau pia wachenjuaji wadogo wa dhahabu”.
Kwa upande wake Afisa Utumishi wa Kiwanda hicho Bw. Philip Sylivanus amesema wanamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri na kuvutia Wawekezaji, wamekuwa wakifanya kazi zao kwa urahisi hususani wakati wa kusafirisha malighafi na bidhaa zao.
Awali kabla ya kutembelea Kiwandani hapo Mkuu wa Mkoa pia alipata wasaa wa kutembelea na kukagua maendeleo katika Kiwanda Kipya cha Pepsi SBC kilichopo Nyakato Industrial Area, Wilayani Ilemela na kupongeza juhudi hizo za uwekezaji mkubwa uliofanywa na kiwanda hicho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.