SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKTA BINAFSI MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na Sekta binafsi Mkoani Mwanza na kusaidia upatikanaji wa huduma na mahitaji mbalimbali yanayotakiwa na Sekta hiyo.
Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo leo Mei 10, 2025 alipotembelea Kiwanda kipya cha kuzalisha vifaa vya migodini cha Rock Solution kilichopo Mayolwa, Usagara, Wilaya ya Misungwi na kumpongeza Mwekezaji kwa uwekezaji mkubwa alioufanya.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wewe kwa sababu ni mzalendo lakini pia uwekezaji huu si kwa ajili ya familia yako lakini watu 300 wataajiriwa hapa”. Amesema.
"Na ndio maana serikali inapambana kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa Sekta binafsi kwa kuwa itaisaidia Serikali kupatikana kwa ajira rasmi na zile ambazo sio rasmi. Ameongeza Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na hayo Mhe. Mtanda ametoa wito kwa Uongozi wa Kiwanda hicho pamoja na Wawekezaji wengine wa Mkoa wa Mwanza kufika Ofisi za Serikali wanapokuwa na jambo au changamoto yoyote inayohitaji ufumbuzi.
“Nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi na uzalishaji wa ajira za wananchi, milango ya Ofisi iko wazi wakati wowote mnakaribishwa”. Amesema Mkuu wa Mkoa.
Akisoma Taarifa ya Kiwanda hicho, Meneja wa Kiwanda cha Rock solution Bw. Fabian Mayenga amesema wameamua kufungua kiwanda hicho ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya viwanda nchini na upatikanaji wa ajira.
Kiwanda hicho ambacho kimejizatiti katika uzalishaji wa vifaa vinavyokwenda kutumika migodini ikiwemo nyavu zinazotumika kuzuia maporomoko ya ardhi chini ya migodi, na sasa wapo katika hatua za ufungaji wa mitambo na mara watakapoanza uzalishaji wanatarajia kutoa ajira zaidi ya 300 za moja kwa moja na zisizopungua 500 zisizo za moja kwa moja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.