Serikali imeeleza dhamira yake ya kupanua masoko ya dhahabu kimataifa kwa kuhimiza viwanda vya kuchakata dhahabu kupata ithibati za kimataifa zitakazowezesha bidhaa hiyo kuuzwa katika masoko makubwa duniani.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb), amekitaka kiwanda cha kuchakata dhahabu cha Mwanza Precious Gold Refinery kufuatilia ithibati ya kimataifa ya London Bullion Market Association (LBMA) ili kuongeza fursa ya kufikia masoko ya dhahabu ya kimataifa.

Mhe. Chaya ametoa wito huo leo Januari 5, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya viwanda na uwekezaji Mkoani Mwanza, ambapo alitembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Ilemela.

Amesema kupata ithibati hiyo kutaiwezesha Tanzania kuongeza ushindani katika soko la kimataifa la dhahabu, kuongeza thamani ya madini hayo na kukuza mapato ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chaya ameielekeza Wizara ya Madini kuanzisha vituo vya pamoja vya kutoa huduma za ununuzi na uuzaji wa madini katika maeneo ya mipakani ili kurahisisha shughuli za kibiashara na kupunguza usumbufu kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.

“Tunawaelekeza wataalamu wa wizara kuanzisha one stop facilitation centers mipakani ili kupunguza usumbufu na kuwavutia wawekezaji wanaokuja kununua dhahabu nchini,” amesema Mhe. Chaya.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Ameir Mkalipa amesema uwepo wa kiwanda cha kuchakata dhahabu umekuwa chachu ya kukuza uchumi wa Mkoa huo kupitia shughuli za uzalishaji, kuongeza mapato na kutoa ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Wakili Mudrikat Kiobya, ameiomba Serikali kuondoa tozo ya asilimia moja kwa wawekezaji wa madini huku akisema hatua hiyo itaongeza ushindani na kuvutia wawekezaji zaidi.

Aidha, ameshauri ofisi zote zinazohusika na biashara ya madini ziwekwe katika kituo kimoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kwa haraka na ufanisi zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.