Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda amesema Serikali inaendelea kufanya uchunguzi kwa shule zote nne zilizobainika kufanya udanganyifu wa mitihani ya kidato cha nne mwaka 2022 na wahusika wote watakao bainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
Akizungumza leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na wazazi wa wanafunzi 140 wa shule ya Sekondari ya Thaqafa waliofutiwa matokeo yao,Mhe.Mkenda amesema vitendo hivyo havitavumiliwa la kuja kuwa na Taifa la watu wasio na weledi na wasomi wababaishaji.
Kuhusu ombi la wazazi hao la kutaka watoto wao kurudia mitihani,Waziri Mkenda amesema kwa sasa hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja kutokana na suala hilo kuwa la kibajeti zaidi na Baraza la Mitihani la Taifa halina fungu hilo kwa sasa hivyo wampe muda wa kuzungumza na wasaidizi wake Wizarani na baadaye Serikali itakuwa na jibu la kuwapa.
Aidha amewashauri wazazi wanaowasomesha watoto wao kwenye shule hizo nne ambazo ni Mnemonic ya Zanzibar,Thaqafa kutoka Mwanza,Cornelius ya Dar es Salaam,na Twibhoki kutoka Mara wajitathmini kama watoto wao wanastahili kuendelea kusoma kwenye shule hizo kabla ya hatua za kinidhamu hazijachukuliwa na Serikali.
"Wazazi wenzangu awali ya yote poleni sana, natambua mlivyo umizwa na jambo hili,Kamishna wa Elimu Dkt.Lyabwene Mutahaba na timu yake wapo katika hatua za uchunguzi kwa shule hizo na hatua itakayofuatia ni kuzifutia usajili ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na mmomonyoko huo wa maadili" Prof.Adolph Mkenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima amewataka wazazi hao kukaa chini na watoto wao ili wawaambie ukweli mienendo ya walimu wao kutokana na kuendelea mambo ya ovyo sana huko shuleni vikiwemo vitendo vya Uzalilishaji kijinsia na ngono.
"Ofisi yangu na Idara ya Elimu ipo wazi kupokea taarifa yoyote inayohusiana na matendo ya ovyo yanayofanywa na baadhi ya walimu wasio na maadili yakiwemo udanganyifu wa mtihani na ngono sitakuwa na huruma kwa watakaobainika zaidi ya kuwafikisha kwenye vyombo vya dola"Mkuu wa Mkoa.
"Mhe.Waziri tunaamimi nawe ni mzazi tumeguswa sana na udanganyifu huu uliofanyika ambao umeingia kutugharimu sisi wazazi, tunakuomba sana utufutie machungu haya kwa kuwaruhusu watoto wetu kurudia mitihani yao" Patrick Masagati Mwenyekiti wa Wazazi shule ya Thaqafa.
Jumla ya wanafunzi 162 walifanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne shule ya Sekondari Thaqafa mwaka 2022 na wanafunzi 22 matokeo yao yalitoka na 140 kufutiwa baada ya kubainika kufanya udanganyifu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.